WANANCHI wa kitongoji cha Kishenge kilichoko kijiji cha Bweyunge Kata ya Kanyigo,wilayani Missenyi,mkoa wa Kagera,wamefanikiwa kujenga barabara ya km 1.5 katika kitongoji hicho,ambayo haikuwepo kabla,na hivyo tangu kuumbwa kwa dunia,hakuna gari limewahi kufika kitongojini hapo.
Sehemu ya baadhi ya wanakitongoji Kishenge,wakiwa katika shughuli ya kusafisha barabara inayolimwa
Na Mutayoba Arbogast,Bukoba
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kitongoji hicho,Jackson Kyalakishaija,wananchi baada ya kukerwa na adha ya kutokuwa na barabara,na hivyo kuwa kama wako kisiwani huku wakihangaika kupata mahitaji muhimu na hata kususiwa kutembelewa na ndugu na marafiki,hivyo wakaona hapana budi kujikwamua kwa kuamua kutoa michango ya fedha na nguvu kazi.
Kwamba liliundwa grupu la WhatsApp la KISHENGE MPYA lililowaunganisha wanakitongoji wazawa walioko mikoa mbalimbali,kuchangia kulima barabara.
Kitongoji hicho kina kaya 97 na kila kaya imechangia sh 5,000 huku walioko nje wakichangia zaidi hata wengine kuchangia hadi sh milioni mbili kwa mtu.
Zaidi ya sh milioni 9.6 imepatikana,na pamoja na mambo mengine,wakafanikiwa kukodi gereda,ambalo linaendelea na shughuli,huku wananchi wakiendelea kusafisha barabara kwa kuondoa mawe na takataka nyingine,na shughuli nyingine za msaragambo,wakiendelea kusubiri nguvu ya serikali.
"Wanakitongoji tulikubalina kwenye mkutano,hakuna anayedai fidia ya kuchukuliwa ardhi yake wala kuharibiwa mashamba,kwa hivyo kila mtu yuko tayari kwa ajili ya maendeleo ya Kitongoji chetu",amesema Kyalakishaija.
Mwanakitongoji Bi Joyce Edson,amesema hakuna gari limewahi kukanyaga kitongojini hapo tangu kuomba kwa dunia kwa kuwa wako bungeni wakizungukwa na vilimavilima vyenye muamba,na upande wa chini zaidi wanapakana na ardhi oevu,pia ziwa Victoria,lakini angalau sasa magari yataanza kuingia.
Mfanyabiashara kitongojini hapo,Paulo Daki,amesema sasa wanakijiji watapata fursa ya kufanya biashara,na wakulima kuuza mazao ya kilimo na misitu,lakini pia kurudisha mahusiano ya ndugu na jamaa waliokuwa wakiona ni 'mzigo' kutembelea kitongoji chao.Ameongeza kusema kuwa hata wagonjwa mahututi waliokuwa wakibebwa kwa machela sasa nitakuwa hivyo tena.
"Tunaiomba Halmashauri ya wilaya ya Missenyi,ituunge mkono nguvu zetu zitakapoishia kwa kutuingiza kwenye mpango TARURA ili barabara yetu iwe katika kiwango cha kupitika majira yote ya mwaka",amesema Daki.
Wanakitongoji hao, kwa namna ya pekee wamemshukuru mwl Mugisha Yusto,anayefanya kazi nje ya wilaya,kwa uhamasishaji mkubwa hadi kufikia hatua hiyo,itakayowafungua toka lindi la kudumaa kimaendeleo.
Gereda likiwa kazini ndani ya kitongoji hicho
Kitongoji hicho cha Kishenge upande wa Mashariki kimepakana na ziwa Victoria,licha ya faida kadhaa za ziwa,bado usafiri ilikuwa tatizo kutoka na kuingia kitongojini hapo.
Safi sana wananchi wa kitongoji hicho! Hakika ni mfano wa kuigwa! Serikali ya wilaya ya Misenyi iwaangalie kwa hicho la pekee wananchi hao.
ReplyDelete