VIGOGO WATATU CHAMA CHA MPIRA WA MIGUU KAHAMA (KDFA) WAFUKUZWA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday, 3 September 2022

VIGOGO WATATU CHAMA CHA MPIRA WA MIGUU KAHAMA (KDFA) WAFUKUZWA



MKUTANO mkuu wa dharura chama cha soka wilayani Kahama mkoani Shinyanga (KDFA) umeazimia kuwafukuza viongozi watatu akiwemo aliekuwa katibu Mkuu wa chama hicho Fadhil Kipindula.


Na Paschal Malulu-Huheso digital


Wengine waliofukuzwa katika mkutano mkuu huo ni aliekuwa kaimu mwenyekiti na makamu mwenyekiti ndugu Tito Okuku Obata sambamba na mwakilishi wa Vilabu Ndugu Donald Igulu.


Mkutano mkuu wa dharura wa chama cha mpira wa miguu wilaya ya Kahama KDFA umefanyika leo Septemba 03, 2022 katika uwanja wa taifa ukiwa jumla ya agenda 9 ambazo ni:- Kufungua kikao, Kuhakiki akidi, Hotuba ya mwenyekiti chama cha soka mkoa, mapato na matumizi, mkataba ligi ya wilaya Kahama na fedha kutopelekwa benki kwa siku husika.


Zingine ni Viongozi wa KDFA kukosa sifa ya Elimu kidato cha nne, kamati ya uchaguzi Shirefa kutangaza na kusimamia kujaza nafasi zote ndani ya KDFA, Mengineyo na kufunga mkuatano.


Hatua hiyo ya kufukuzwa viongozi hao ni kutokana na kubainika kuna ubadhirifu wa fedha na matumizi mabaya ya ofisi iliyopelekea viongozi hao watatu kuwatenga wajumbe wengine wa kamati tendaji na kusababisha upotevu wa fedha za chama sambamba na kuhamisha nyaraka za chama ndani ya ofisi na kutembea nazo kwenye begi.


Tuhuma zingine zilizopelekea kufukuzwa mamlakani viongozi hao ni kutoshirikiana na viongozi wengine wa kamati tendaji ya KDFA katika vikao baada ya tuhuma za upotevu wa fedha Zaidi ya millioni nne kuripotiwa kuliwa na viongozi wachache.


Baada ya majadiliano mkutano huo uliamua kupiga kura ya siri kwa mujibu wa katiba ambapo kura hizo ziliamua kuwafukuza katika madaraka ndani ya chama hicho huku wajumbe wakiazimia fedha zilizopotea kurejeshwa ambapo ni milioni 2.2 ambazo aliekuwa katibu amekiri kuzitumia kinyume na utaratibu wa chama ambapo ameahidi Oktoba 03, 2022 atakuwa amerejesha.


Baada ya kupigwa kura hizo ambapo jumla ya wanachama 59 waliohudhuria kutoka vilabu mbalimbali wilayani Kahama aliekuwa katibu amepata kura 57 zakutokuwa na Imani nae huku akipata kura 2 za kuwa na imani nae sambamba na Donald Igulu pamoja na Tito Okuku Obata hivyo kufukuzwa rasmi.


Aidha mkutano huo umeiagiza kamati tendaji ikiongozwa na kaimu mwenyekiti ambaye ni mjumbe wa muda mrefu ndani ya KDFA Hamis Shilinde kuhakikisha ndani ya siku 30 uchaguzi ufanyike kuziba nafasi zilizowazi ambazo ni:- Mwenyekiti KDFA, Makamu mwenyekiti, katibu mkuu, mjumbe wa vilabu na mjumbe mkutano mkuu nafasi iliyokuwa wazi baada ya mjumbe kujiuzulu.


Pia wanachama kupitia mkutano mkuu huo wameiagiza kamati tendaji hiyo kuhakikisha inafuatilia fedha zote za KDFA kwenye vyanzo vyake na kuhakikisha watuhumiwa hao wanarejesha fedha hizo itakapobainika.


Akitoa neno la shukrani Mwinyi Eliasa ambaye ni katibu wa vilabu amesema hatua hiyo ni ya kidemkrasia kwani kila mtu amepata haki yake na wao maamuzi waliyoyafanya ni kwa ajili ya maendeleo ya mpira wa miguu.


Kwa upande wake kaimu mwenyekiti Hamis Shilinde amewahikishia wanachama wa KDFA kuwa ndani ya siku 30 uchaguzi wa nafasi zilizowazi utakuwa umefanyika huku akiomba ushirikiano wa kutoka kwa wanachama hao.


Mmoja ya viongozi waliofukuzwa Tito Okuku amesema hatua hiyo kufikiwa sio mbaya na hana kinyongo na mtu kwani ameponzwa na wachache katika utekelezaji wa majukumu yao ipasavyo.


Mkutano mkuu huo wa dharura ulioitishwa kwa nguvu ya vilabu ulikuwa umehudhuriwa na Kamati tendaji ya Shirefa ikiongozwa mwenyekiti wake Said Mankiligo, Mjumbe wa kanda namba nne TFF, Mohamed Aden na kamati ya uchaguzi Shirefa.


MWISHO

1 comment:

Post Top Ad

Pages

Huheso