Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote umewasilishwa bungeni ambapo mwajiri wa sekta ya umma na binafsi rasmi atapaswa kumsajili mwajiriwa katika skimu ya bima ya afya ndani ya siku 30 tangu kuanza kwa mkataba wa ajira.
Muswada huo uliosomwa kwa mara ya kwanza leo, Ijumaa Septemba 23,2022, utakwenda kujadiliwa katika kamati kabla ya kumalizia mchakato mwingine wa utungaji wa sheria.
Pamoja na mambo mengine unatoa masharti ya mwajiri wa sekta ya umma na sekta binafsi kuwasilisha katika skimu asilimia sita ya mshahara wa mwajiriwa, ambapo ndani yake mwajiri atachangia nusu au zaidi ya kiwango hicho, na kiwango kilichosalia kitachangiwa na mwajiriwa.
Aidha, waziri kwa kushauriana na waziri mwenye dhamana ya masuala ya fedha, ataainisha viwango vya uchangiaji kwa ajili ya sekta isiyo rasmi, kama itakavyoainishwa katika kanuni, kwa kuzingatia tathmini ya uhai na uendelevu wa skimu za bima ya afya katika utoaji wa kitita cha mafao ya msingi.
No comments:
Post a Comment