MWENYEKITI wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation ya mjini Kahama mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja amekitahadharisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kiache kujiona ni chama bora kuliko vyama vingine vya siasa.
Mwenyekiti huyo ameelezea kushitushwa kwake na tamko la vitisho ambalo limetolewa na CHADEMA hivi karibuni lenye viashiria vya vitisho kwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juzi, Mgeja yeye binafsi ameshitushwa na kusikitishwa na tamko la chama hicho ambalo linaashiria kuleta uchochezi na uvunjifu wa amani na halikuzingatia misingi ya utawala bora unaoheshimu sheria.
Mgeja ambaye ni miongoni mwa makada wenye misimamo ndani ya Chama Cha Mapinduzi alisema Taasisi anayoiongoza yeye haitakubali kukivumilia Chama chochote cha kisiasa, kikundi au mtu ye yote anayejihusisha na utoaji wa matamko yenye viashiria vya vurugu, uchochezi yanayoweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Alisema matamko ambayo yametolewa na Kamati Kuu ya CHADEMA yakiipa CCM na Serikali yake masharti manane yanaonesha ni aina ya vitisho na yamekosa subira na hayazingatii suala la utawala bora wa kisheria.
“Mimi naomba ndugu niwaeleze wazi, ni vyema CHADEMA itambue hii Tanzania ni ya watanzania wote na kama ni uzalendo pia unamgusa kila mtanzania, kwa hiyo wao kuonekana ndiyo chama pekee kinachopigania haki ya watanzania siyo kweli,”
“Ni vizuri wakatambua kuwa hata vyama vingine vya kisiasa hapa nchini pia ikiwemo chama tawala CCM vyote vinapigania haki na maendeleo ya watanzania tena kwa kuzingatia misingi ya utawala bora unaozingatia sheria,” alieleza Mgeja.
Mwenyekiti huyo ambaye miongoni mwa kazi zinazofanywa na taasisi yake ni suala la utawala bora, haki na demokrasia alisema suala la mikutano ya hadhara na Katiba mpya siyo takwa la CHADEMA peke yake bali hata vyama vingine ikiwemo CCM yenyewe vinamahitaji hay ohayo.
Alisema tofauti na CHADEMA vyama vingine vyote vya siasa hapa nchini vinahitaji michakato ya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na katiba mpya utekelezwe kwa utaratibu mzuri na yawepo maridhiano ya watanzania wote tena kwa kuheshimu misingi ya sheria.
“Nichukue fursa hii kukipongeza Chama cha Mapinduzi (CCM) chini ya mwenyekiti wake Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kukaa meza moja ya mazungumzo na CHADEMA ambayo yatapelekea kupatikana kwa maridhiano, na nimpongeze vilevile kwa kuunda Kikosi Kazi cha kupitia maoni mbalimbali kuhusu suala la katiba,” alieleza Mgeja.
Katika hatua nyingine Mgeja alikiomba na kukipa ushauri wa bure chama hicho cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwamba kiitumie fursa iliyotolewa na Rais Samia ya maridhiano ya pamoja kwa manufaa mapata ya Taifa la Tanzania kuliko kuonesha dalili za kutaka kuweka mpira kwapani.
Pia amevipongeza vyama vyote vya siasa nchini ikiwemo CCM kwa kuendelea kuwa na subira kukipa nafasi kikosi kazi kilichoundwa na Rais ili kifanye kazi yake vizuri na mwisho ni wazi kwamba watanzania wote watatangaziwa matokeo ya kazi inayoendelea kufanyika hivi sasa.
“Niwaombe watanzania tuendelee kuwa na subira na kujiepusha na upotoshwaji, uchochezi na mashinikizo yoyote yanayotolewa na CHADEMA, tuendelee kuheshimu suala la utawala wa kisheria na utii wa sheria pasipo shurti,”
“Hata hili suala la wabunge kumi na tisa wa viti maalumu wa CHADEMA ni wazi lipo nje ya uwezo wa CCM na Serikali yake, tusiwabebeshe lawama, tuwe na subira na tuuachie mhimili husika (mahakama) itekeleze wajibu wake wa kisheria, tusishinikize uvunjifu wa sheria za nchi,” alieleza Mgeja.
No comments:
Post a Comment