Kijana Hamisi Said Kibunda (34) mkazi wa Kata ya Kilolambwani, Tarafa ya Mchinga, mkoani Lindi, amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 gerezani pamoja na kuchapwa viboko 12, baada ya kukutwa na hatia ya wizi fedha kiasi cha shilingi milioni 3 kwa kutumia silaha.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya hiyo, Maria Batraine, baada ya kuridhishwa pasipo shaka na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mshtakiwa alipewa nafasi ya kujitetea na kuiomba Mahakama imuonee huruma kwa kutompa adhabu kali akidai ni kijana anayehitajika kutumika kujenga uchumi wa Taifa lake na kwamba anayo familia inayomtegemea akiwemo mke, mtoto na wazazi aliyedai ni wazee, hivyo kama atapewa adhabu kali watakosa huduma zake.
Baada ya utetezi huo,Hakimu Batraine akamuuliza Mwanasheria wa Serikali, Rabia Ramadhani,iwapo ana kumbukumbu ya makosa ya zamani kwa mshtakiwa na kujibu hana, huku akiiomba Mahakama kumpa adhabu kali ili iwe fundisho kwake na wengine walio na tabia ya aina hiyo.
Rabia alidai kitendo cha kutumia silaha husababisha mazingira na hasara kubwa ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
CHANZO:EATV
No comments:
Post a Comment