Jeshi la Polisi Mkoani hapa linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kujihusisha kwa kujifanya maofisa kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kisha kuwaibia wastaafu.
Akizungumza Agosti 27, 2022 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Martin Otieno amesema watuhumiwa hao wamefanya wizi huo katika mikoa mbalimbali nchini kwa kuwataka wastaafu wawape fedha ili wawasaidie kulipwa mafao yao kwa haraka.
Kamanda Otieno amesema mbinu wanazotumia wezi hao ni kukusanya taarifa za wastaafu, kujifanya maafisa wa PSSSF na Tamisemi na kusajili laini za simu bandia.
“Watuhumiwa hao wamekamatwa na nyaraka saba za Serikali zenye taarifa za wastaafu na namba zao za simu, mashine saba za Famoco (mashine za kusajilia laini za simu) na laini zilizoharibiwa kwenye mfumo elekezi wa kusajili laini,” amesema Otieno.
Aidha amesema walikuta laini za simu 103 zilizosajiliwa na kutumika kiuhalifu na laini 168 ambazo hazijasajiliwa, vitambulisho vya watu mbalimbali na simu 11 za mawasiliano maalumu na watu waliowaweka katika mtego wa kuwatapeli.
No comments:
Post a Comment