WAHAMIAJI ZAIDI YA 2000 WALIOKAMATWA KAGERA WARUDISHWA MAKWAO WENGINE WAPANDISHWA KIZIMBANI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Thursday, 4 August 2022

WAHAMIAJI ZAIDI YA 2000 WALIOKAMATWA KAGERA WARUDISHWA MAKWAO WENGINE WAPANDISHWA KIZIMBANI



 
Jumla ya wahamiaji haramu 2,935 wamekamatwa na idara ya uhamiaji katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kagera, katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu, baada ya kubainika kuingia nchini bila vibali


Akizungumza na waandishi wa habari Kamishna msaidizi idara ya Uhamiaji Mkoani Kagera, Thomas Fussy amesema kuwa wahamiaji hao haramu wamekamatwa kufuatia oparesheni mbalimbali zinazoendelea kwa lengo la kuwabaini watu hao, na kuwachukulia hatua za kisheria.


"Wahamiaji haramu waliokamatwa kutoka Burundi ni 2,389, Uganda 308, Rwanda 175, Kongo 40, Kenya 10, Ethiopia watano, Somalia watatu, China watatu na Zambia na Zimbabwe mhamiaji mmoja kwa kila nchi, kati ya watuhumiwa hao wahamiaji 2,730 waliondoshwa nchini, 183 wamefikishwa mahakamani na 22 wamehalalisha ukazi wao hapa nchini na kulipa ada kwa hati maalumu" amesema Fussy.


Aidha kutokana na mkoa wa Kagera kupakana na nchi nyingi na kusababisha kuwepo kwa mwingiliano wa watu kutoka katika mataifa hayo, kamishna huyo msaidizi wa idara ya uhamiaji mkoani Kagera amewataka watendaji wa vitongoji, vijiji na mitaa, kutotoa barua za utambulisho kwa wananchi ambao hawana uhakika kama ni wakazi wa maeneo yao, ili kuepuka kutoa nyaraka za serikali kwa watu wasio raia.


"Kwa hiyo mtendaji asikubali kutoa nyaraka kwa mtu ambaye hajamfahamu kwa sababu nyaraka zinaishi, na akiulizwa popote ataonyesha hizo nyaraka na ikibainika sio raia atachukuliwa hatua yeye, na wewe uliyesaini utawajibishwa" amesema Fussy


Nao baadhi ya wananchi waliozungumzia suala hilo wameiomba serikali kupitia mamlaka zake ikiwamo idara ya usalama wa taifa na uhamiaji, kuongeza umakini kuwadhibiti watu wasio raia kuingia nchini bila utaratibu, wakidai wao kama wananchi sio rahisi kuwabaini.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso