SIKU chache baada ya wanachama zaidi ya 400 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Mahina wilayani Nyamagana mkoani Mwanza, kutishia kurudisha kadi za chama hicho kutokana na kasoro mbalimbali za uchaguzi wa mashina 80 na matawi manane katika eneo hilo umefutwa rasmi.
Miongoni mwa kasoro zilizolalamikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi huo kwa kuteua viongozi badala ya kuwachagua kama kanuni za CCM zinavyoelekeza.
Akizungumza jana Katibu wa CCM Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Geofrey Robert, alisema uchaguzi huo umefutwa baada ya kuwapo malalamiko ya ukiukwaji wa kanuni zinazosimamia uchaguzi.
Alisema licha ya kuwapo malalamiko katika kata zingine wilayani humo, lakini Kata ya Mahina yalikuwa mengi ndiyo maana walichukua hatua haraka na utafanyika baada ya kukamilika taratibu za ndani.
Kutokana na hatua hiyo, Robert alisema uchaguzi ngazi ya kata hiyo hautafanyika kama ilivyopangwa hadi hapo uchaguzi wa mashina na matawi utakapofanyika.
"Kanuni za uchaguzi zilikiukwa kwa kiasi kikubwa katika uchaguzi ule na wanachama wetu walilalamika na kwa kuwa sisi ni chama kikubwa tuliamua kuchukua hatua hii," alisema Robert.
Hali hiyo imejitokeza ikiwa ni miezi minne tangu uongozi wa CCM Taifa kupiga marufuku upangaji wa safu za uongozi ndani ya chama hicho kwa kuangalia uchaguzi mkuu wa 2025.
Aprili 10, mwaka huu, Makamu Mkwenyekiti wa CCM Taifa, Abdulrahman Kinana na Katibu Mkuu wake, Daniel Chongolo, waliwataka wanachama wanaopanga safu kuacha mara moja kwa kuwa hawatafanikiwa na hatua zitachukuliwa dhidi yao.
Walisema viongozi wanaopanga safu ya watu wanaowataka hawana nia njema ya kusukuma gurudumu la maendeleo mbele, huku wakisisitiza ni haki ya mwanachama kuchagua na kuchaguliwa.
Licha ya uchaguzi huo kufutwa, baadhi ya wanachama wa eneo hilo walioulalamikia wamedaiwa kuitwa katika kamati za maadili na kutishwa, huku wakidai kupangwa kwa safu za uongozi jambo ambalo ni kinyume na kanuni.
Akizungumzia suala hilo, Robert alisema kila mwanachama ana haki ya kusikilizwa na kwamba haki lazima itendeke kwa kufuata kanuni na taratibu za uchaguzi na siyo kutishwa.
Wiki iliyopita wanachama wa CCM katika kata hiyo akiwamo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi katika Kata ya Mahina, Patrick Brakari, alisema uchaguzi huo ngazi ya mashina na matawi umeshafanyika katika maeneo mengine, lakini wameshangaa kuona viongozi walipatikana kwa kuteuliwa badala ya kuchaguliwa.
Aidha, alisema haijulikani nani aliteua viongozi hao kwa kuwa kama kiongozi wa kata hajawahi kuona wala kushiriki chaguzi hizo, na hajui walipatikanaje.
Aliongeza kuwa kutokana na sakata hilo, wanachama walikasirika na kutishia kurudisha kadi zao za chama kama haki isingefanyika, ikiwamo kuitishwa uchaguzi kwa kufuata katiba.
Brakari alisema kwenye kata yake ilitolewa fomu moja kwa kila nafasi, hatua inayowanyima wengine nafasi kwa kuonyesha waliojaza wamepita bila kupinga.
Alifafanua kuwa Katiba ya CCM inataka kila mtu apigiwe kura hata kama yupo peke yake, ipigwe kura ya ndiyo ama hapana, lakini kilichotokea wao walipelekewa majina ya wateule ambayo walichagua wenyewe na siyo kuchaguliwa na wanachama.
"Kata ya Mahina kuna rafu za ajabu kabisa, yaani mimi ni kiongozi ngazi ya kata, lakini sijui uchaguzi wa mshina na matawi ulifanyika lini, wapi na ulisimamiwa na nani,” alihoji Brakari.
Kutokana na sakata hilo, alisema yeye pamoja na wanachama wenzake waliandika barua wilayani kulalamika kuhusu sakata hilo.
Aliongeza kuwa kuna viongozi wa ngazi mbalimbali wanapanga safu za wanachama watakaowapigia kura na kwamba hiyo ndiyo sababu kwenye kata hiyo viongozi wa mashina na matawi wameteuliwa badala ya kuchaguliwa.
Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Nyamagana, Zebedayo Athuman, alithibitisha kufahamu mgogoro huo ambao alisema ni wa muda mrefu.
Alipoulizwa kuhusu wanachama kutaka kurudisha kadi za chama kutokana na kuteuliwa viongozi wasiowataka, alisema hahusiki na suala hilo.
Alisema wanachama wa mashina, matawi na kata ya Mahina wilayani Nyamagana walifikisha suala hilo ngazi ya wilaya, ingawa hakutaka kusema uamuzi gani ulitolewa kwa wakati huo.
Uchaguzi wa mashina na matawi ndani ya CCM ulianza Aprili 2, mwaka huu, na sasa unahitimishwa kwa wagombea kupigiwa kura na wanachama halali.
Huyu M/kiti wa wilaya ya nyamagana yuko vizuri
ReplyDelete