Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo Jumatatu Agosti 29, 2022, amemwapisha Kamishna Jenerali wa Magereza, Mzee Ramadhan Nyamka pamoja na majaji 21 wa Mahakama Kuu aliowateua siku chache zilizopita.
Viongozi hao wameapishwa Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu, George Mkuchika na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Eliezer Feleshi.
Kabla ya kumwapisha Nyamka, Rais Samia amempandisha cheo kutoka Kaimu Kamishna wa Huduma za Urekebishaji, Jeshi la Magereza kuwa Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP).
Nyamka amekipokea kijiti hicho kutoka kwa Meja Jenerali Suleiman Mzee ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Anakuwa Kamishna Jenerali wa Magereza wa tano ndani ya miaka 10 akitanguliwa na Joan Minja (2012 – 2017), Dk Juma Malewa (2017 – 2018), Phaustine Kasike (2018 – 2020) na Suleimani Mzee (2020 – 2022).
Mbali na Nyamka, Rais Samia amewaapisha majaji 21 kati ya 22 wa Mahakama Kuu aliowateua Agosti 6, 2022 na baada ya kiapo hicho, wote wakala kiapo cha maadili kwa watumishi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili, Jaji Sivangilwa Mwangesi.
No comments:
Post a Comment