Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Profesa Mark Mwandosya kuwa Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na maji (Ewura)akichukuwa nafasi ya Profesa Jamidu Hazzam ambaye amemaliza muda wake.
Taarifa ya uteuzi huo imetolewa leo Agosti 19, 2022 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Zuhura Yunus na kueleza kuwa uteuzi wake umeanza tangu Agosti 15 mwaka huu.
Mwandosya ambaye alizaliwa mwaka 1949 aliwahi kuwa mbunge wa jimbo la Rungwe Mashariki kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kuanzia Novemba 2000 hadi Julai mwaka 2015.
Pamoja na ubunge pia aliwahi kuwa Waziri katika Ofisi ya Rais (2013-2015), Wizara ya Maji (2010-2013), Wizara ya Maji na Umwagiliaji (2008-2010), Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira (2006-2007) na Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi (2000-2005).
Vilevile amewahi kuwa Katibu Mkuu katika Viwanda na Biashara (1993-1994), Maji, Nishati na Madini (1990-1992) pamoja na Kamishna wa tume ya Nishati na Mambo ya Petrol (1985-1990).
No comments:
Post a Comment