Kiongozi wa mwisho wa uliokuwa Umoja wa Kisovieti Mikhail Gorbachev, amefariki dunia akiwa na miaka 91. Viongozi wa ulimwengu wametuma salamu za pole wakimtaja kuwa na mchango mkubwa katika historia ya ulimwengu.
Gorbachev amefariki dunia jana katika hospitali mjini Moscow kutokana na maradhi ya muda mrefu. Mwanasiasa huyo ambaye alikuwa madarakani kati ya mwaka 1985 hadi 1991, alikuwa ndiye kiongozi wa mwisho wa enzi ya vita baridi.
Atakumbukwa kwa mchango wake wa kumaliza vita baridi bila umwagaji damu lakini akikosolewa kwa kushindwa kuzuia kusambaratika kwa Umoja wa kisovieti.
Mnamo tarehe 25 Desemba mwaka 1991, Gorbachev aliyekuwa ameuongoza Umoja wa Kisovieti kwa miaka saba alijiuzulu wadhifa wake, na bendera ya muungano huo ilishushwa na kupandishwa ile shirikisho la Urusi.
Kuanzia mwaka 1985 hadi kuanguka kwa muungano huo mwaka 1991, Gorbachev alisimamia mageuzi makubwa ya sera za kiuchumi na kisiasa za Urusi.
Alishinda Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 1990 kwa kusaini mkataba wa kihistoria wa silaha za nyuklia na kiongozi wa Marekani wa wakati huo Ronald Reagan. Gorbachev alisema kuwa;
"Vizazi vijavyo vitatoa uamuzi wao juu ya umuhimu wa tukio ambalo tunakaribia kulishuhudia. Lakini nitathubutu kusema kwamba tunachofanya sasa, kusaini makubaliano ya kwanza kabisa ya kuondoa silaha za nyuklia, kuna umuhimu kwa ulimwengu wote binadamu, kutoka katika mtizamo wa siasa za ulimwengu na fikra za ubinadamu."
Mwanasiasa huyo aliungwa mkono katika mataifa ya magharibi kwa kuongoza mageuzi yaliyochochea uwazi na mjadala mkubwa wa umma ulioharakisha kuvunjika kwa himaya ya kisovieti.
Hata hivyo nchini Urusi, kiongozi huyo aligubikwa na utata na kuwa na uhusiano mgumu na rais Vladimir Putin.
Kwa Putin na Warusi wengi kusambaratika kwa Umoja wa Kisovieti, ilikuwa ni jambo la kusikitisha lililochangia muongo mmoja wa umaskini wa Urusi na kushuka kwa hadhi ya nchi hiyo katika uso wa dunia.
Chanzo:DW
No comments:
Post a Comment