Karani wa Sensa ya Watu na Makazi wilayani Bunda mkoa wa Mara amejifungua muda mfupi kabla ya kuanza kazi hiyo, hivyo kulazimika kuondolewa kwenye orodha ya makarani katika wilaya hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Nassari amesema kuwa karani huyo amejifungua usiku wa kuamkia Agosti 23, 2022 ingawa hakuweza kumtaja jina.
"Tangu tumeanza tumepata changamoto ambayo pia ni baraka kuna karani wetu amejifungua usiku na bahati nzuri alijifungua kabla ya saa sita kwahiyo yeye na mtoto wake pia wamehesabiwa na baada ya hali hiyo kujitokeza tayari karani wa akiba ameshachukua nafasi na kazi inaendelea," amesema Nassari.
Amefafanua kuwa wilaya ya Bunda inao makarani zaidi ya 1,000 na kwamba shughuli ya kuhesabu watu na makazi inaendelea na huku akiamini kuwa kazi hiyo itakamilika kwa ufanisi.
Amewataka wakazi wa Bunda kutoa ushirikiano kwa makarani na kutoa taarifa sahihi zitakazowiewezesha serikali kupanga mipango ya maendeleo kwa nchi na wananchi kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment