WATUMISHI REA WASISITIZWA UCHAPAKAZI NA KUZINGATIA WELEDI WA KAZI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Sunday, 31 July 2022

WATUMISHI REA WASISITIZWA UCHAPAKAZI NA KUZINGATIA WELEDI WA KAZI



Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amewataka wafanyakazi wote wa Taasisi hiyo kufanya kazi kwa weledi na kujituma ili kufikia malengo yake ya kuboresha maisha ya wananchi vijijini kwa kuwezesha upatikanaji wa nishati bora na zenye gharama nafuu.


Aliyasema hayo mwishoni mwa juma, Julai 29, 2022 wakati wa kikao maalum baina yake na wafanyakazi wa REA kilicholenga kujadili utendaji kazi, kusikiliza changamoto za watumishi na kuzitolea majibu.


Mhandisi Saidy aliwataka wafanyakazi wote kushirikiana na kuweka nguvu ya pamoja katika utekelezaji wa vipaumbele vya Wakala kwa sasa, ambavyo alivibainisha kuwa ni pamoja na kupeleka umeme vitongojini, programu ya kusaidia upatikanaji wa petroli vijijini, mradi wa kuwezesha upatikanaji wa nishati bora ya kupikia vijijini pamoja na kupeleka umeme katika visiwa.


Kuhusu usambazaji umeme vitongojini, alieleza kuwa ni mradi unaolenga kuvipelekea umeme vitongoji vyote ambavyo havijafikiwa na nishati hiyo, baada ya kila kijiji sasa kufikiwa na mradi wa umeme.


Alifafanua kuwa gharama ya mradi inakadiriwa kuwa shilingi trilioni 6.5 na kwamba katika mwaka huu wa fedha, shilingi bilioni 140 zimetengwa kwa ajili ya utambuzi wa wigo wa mradi pamoja na kuanza kazi ya utekelezaji wa mradi awamu kwa awamu.


Vilevile, aliuelezea mradi wa kuwezesha ujenzi wa vituo vidogo vya kusambaza bidhaa za petroli vijijini, ambapo alibainisha kuwa Serikali imeubuni ikilenga kuwezesha na kuendeleza vituo hivyo kwa maeneo ya vijijini ambayo hayana vituo vya mafuta kwa njia ya mkopo nafuu.


Alisema kuwa mradi huo ni wa majaribio ambao ni sehemu ya jitihada za kutafuta mbinu bora zaidi za kusambaza nishati ya mafuta salama na kwa bei nafuu vijijini.


Pia, Mkurugenzi Mkuu alifafanua kuwa katika mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga shilingi milioni 500 ili kufanya kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati bora ya kupikia pamoja na kuwezesha kufanyika kwa tafiti za kubaini nishati, mfumo sahihi na vivutio vya kusambaza nishati hiyo kwa maeneo ya vijijini.


Aliongeza kuwa, katika mwaka wa fedha 2022/23, shilingi bilioni 10 zitatumika kutekeleza mradi wa majaribio wa kupeleka na kusambaza gesi asilia katika makazi ya wananchi wanaopitiwa na mkuza wa bomba kuu la gesi katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani.


Aidha, kuhusu kipaumbele cha nne kinachohusisha upelekaji umeme visiwani na maeneo yaliyo mbali na Gridi ya Taifa, Mhandisi Saidy alieleza kuwa mradi unahusisha ujenzi wa miradi midogo midogo ili kuzalisha na kusambaza umeme kutokana na vyanzo vya nishati jadidifu kama vile jua, upepo, maporomoko madogo ya maji pamoja na tungamotaka.


Alitaja gharama ya mradi kuwa ni takribani shilingi bilioni 54 na kwamba katika mwaka huu wa fedha, shilingi bilioni 20 zimetengwa kutoka Serikali ya Tanzania.


Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu aliwahakikishia wafanyakazi wa REA kuwa changamoto mbalimbali zinazowakabili, zitaendelea kufanyiwa kazi ili kuzitatua na kuwawezesha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.


Akizungumza kwa niaba ya Wafanyakazi, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), Tawi la REA, Swalehe Kibwana alimshukuru Mkurugenzi Mkuu kutenga muda wa kukutana na wafanyakazi ili kuzungumza nao na kupokea changamoto zao.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso