MASHABIKI na baadhi ya viongozi wa timu pinzani hutoa kauli kali kuponda mpango fulani wa timu pinzani kama kukosa ubora kwa mchezaji aliyesajiliwa, kufanya usajili mbovu au wa kiwango cha chini, kuwa na bajeti ndogo ya usajili nk.
Na Ibrahim Mkamba.
Wasichojua ni kwamba kuponda huko kunawahamasisha wanaopondwa wafanye makubwa kuwaumbua wapondaji.
Subiri Habib Kyombo wa Simba na Gael Bigirimana wa Yanga wakipangwa mechi ya ngao watakavyopambana kuwaumbua wanaowaponda sasa.
Kama tajiri wa timu pinzani amepunguza bajeti ya usajili, hiyo ni faida kwenu wapinzani wa timu hiyo. Mkiuponda uamuzi wake huo mtamfanya abadili uamuzi wake na kuongeza kwa kiasi kikubwa fungu hilo. Ni kama vile mmemtaka aongeze bajeti hiyo kwa manufaa ya timu yake ambayo ni pinzani na ya kwenu. Uhamasishaji huu kwa tajiri wa wapinzani wenu una faida gani kwa timu yenu?
Msimu uliopita, Simba walikuwa wasifanye tamasha la Simba Day kutokana na kubanwa na ratiba ya maandalizi ya msimu. Bwana Haji Manara alipoipata kiuhakika habari hiyo, akawa akiwaponda Simba kwa nguvu hadharani kwamba wameshindwa kuandaa Simba Day. Kwa kuponda huko, aliwahamasisha waliandae tamasha hilo, wakaliandaa na likafana!
USHAURI: Kama ni lazima kuwaponda wachezaji wa timu pinzani, subirini kwanza muuone utendaji wao uwanjani. Unapondaje mchezaji wa timu pinzani kabla hujamuona anavyochezea timu yake mpya?
Pili, kuna tija kubwa kuzungumzia zaidi mipango ya timu yako badala ya kutumia muda wowote kuwaponda wapinzani kuwasaidia kuweka sawa mambo yao kukuumbua.
Kuweni professional kama Senzo Mbatha wa Yanga ambaye ukimsikia anaongea, utamsikia anaizungumzia Yanga yake. Hutamsikia hata siku moja akizungumza kuhusu Simba alikotoka.
No comments:
Post a Comment