Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema amefunga mafunzo ya Walimu wa Makarani na Wasimamizi wa Sensa ya Watu na Makazi 2022 mkoa wa Shinyanga huku akiwasisitiza wahitimu hao wa mafunzo kuwa wazalendo na kuepuka kuwa wakali kwa wananchi.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mafunzo hayo yaliyodumu kwa siku 21,2022 yamefungwa leo katika Ukumbi wa Chuo cha Ualimu SHY COM Mjini Shinyanga yakihusisha washiriki 194.
“Nendeni mkamalize kazi, kafundisheni yale mliyofundishwa. Msiende kupotosha jamii kuhusu sensa ya watu na makazi bali nendeni mkafanye kazi kwa uzalendo na umakini mkubwa ili sensa ya watu na makazi iwe na mafanikio”,amesema Mjema.
“Msiende na ya kwenu,nendeni mkatumie madodoso mliyofundishwa. Muwe wapole mnapoongea na wananchi. Usiwe mkali kama mwananchi hafunguki unapomuuliza”,ameongeza Mjema.
Ametumia fursa hiyo kuwataka viongozi na wadau mbalimbali kuendelea kutoa elimu ya sensa ya watu na makazi huku akibainisha kuwa mkoa wa Shinyanga umejipanga kikamilifu kufanikisha zoezi la sense ya watu na makazi Agosti 23,2022.
“Kazi iliyobaki sasa ni kulipiga debe la sensa hadi kieleweke. Ukiwa na mkeo au mmeo huko nyumbani mwambie kuhusu Sensa, tuongeze juhudi za kutoa elimu ya sensa na makazi”,amesema.
Mratibu wa Sensa ya Watu na Makazi Mkoa wa Shinyanga, Eliud Kamendu amesema mafunzo ya Makarani, Wasimamizi wa Maudhui na wasimamizi wa TEHAMA mkoa wa Shinyanga yaliyofanyika kwa siku 21 yalianza Julai 6,2022 na yatafikia tamati Julai 26,2022 yakiwa na jumla ya washiriki 194 kati yao makarani 184, wakufunzi 7, mratibu msaidizi wa sense mkoa na mratibu wa sensa mkoa.
“Mafunzo haya yalianza kutolewa kwa kufundisha Dodoso la Jamii, Dodoso kuu la sense, dodoso la makundi maalumu, dodoso la majengo na miongozo mbalimbali ya wakufunzi, wadhibiti ubora na waratibu wa sensa ngazi ya wilaya. Hali kadhalika mafunzo haya yalijumuisha kwenda uwandani kujifunza kwa vitendo mambo yote yaliyofundishwa darasani katika madodoso yote sambamba na kufanya majaribio kwa makarani”,amesema Kamendu.
“Mafunzo haya yamefanyika katika ubora wa hali ya juu na timu hii imekuwa timu ya ushindi ambayo itakwenda kuwafundisha vyema makarani, wasimamizi wa maudhui na wasimamizi wa TEHAMA ngazi ya wilaya kuanzia Julai 29,2022 hadi Agosti 16,2022 kwa ustadi mkubwa ambao ndiyo watakaokwenda kutekeleza zoezi zima la sense ya watu na makazi kwa mwaka 2022”,ameeleza Kamendu.
No comments:
Post a Comment