WAFANYAKAZI wanaokaa kwenye viti kwa muda mrefu ofisini, wapo hatarini kuvimba miguu kutokana na kubana mishipa ya damu.
Wameshauriwa kujenga tabia ya kusimama na kufanya mazoezi ya kunyoosha mwili ili kujiepusha kubana mishipa hiyo. Mtaalamu wa Udhibiti wa Magonjwa wa Wizara ya Afya, Dk. Baraka Nzobo, akizungumza na Nipashe jana, alisema wafanyakazi hususani Makatibu Mahsusi ambao wanakaa zaidi ya saa tatu wanapaswa kutenga muda kidogo wa kutembea ili kuipa nafasi mishipa ya damu kufanya kazi vizuri.
“Kiafya sio vyema mtu kukaa chini zaidi ya saa tatu unapaswa kusimama na kutembea kidogo ili kuipa nafasi mishipa ya damu kufanya kazi yake vizuri ya kusambaza damu na kuepusha tatizo la kuvimba miguu,” alisema.
Hata hivyo, Dk. Nzobo alisema, mazoezi ya kufanya sio kukimbia pekee, kutembea ni mazuri hususani kwa mtu ambaye hajawahi kufanya mazoezi. “Unaweza kuanza na mazoezi ya kutembea umbali mfupi na kadri siku zinavyozidi kwenda unaongeza umbali wa kutembea na mwili ukitoa jasho basi umefanya mazoezi ya kutosha,” alisema Dk. Nzobo.
Aliiasa jamii kutambua umuhimu wa kufanya mazoezi kwa muda mchache na baadaye kuendelea na shughuli mbalimbali za ujenzi wa taifa.
“Naomba jamii iwe inafanya mazoezi mara kwa mara ya kusimama, kutembea na wenye uwezo wa kufanya mazoezi ya kukimbia bado yanaruhusiwa na hiyo yote ni kujiweka mwili sawa,” alisema Dk. Nzobo.
Mmoja wa wakazi wa Dodoma, Julieth Mosha, alisema amekuwa akifanya mazoezi kila siku ili kuhakikisha afya yake inakuwa vizuri na anafanya ya kutembea pamoja na kukimbia.
Alisema tangu ameanza kufanya mazoezi hayo kwa kufuatilia ushauri wa wataalamu, afya imeimarika ikiwamo kufanikiwa kupunguza uzito uliokuwa hauendani na umri wake.
Alishauri jamii kujiwekea utaratibu wa kufanya mazoezi kila mara ili kujiepusha na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
No comments:
Post a Comment