Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini imeitaka Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), kuweka nguvu katika ujenzi wa barabara za mawe kwa kuwa zinadumu na gharama za ujenzi wake ni nafuu.
Hayo yalielezwa jana na Makamu Mwenyekiti wa bodi hiyo, Octavian Mshiu alipokagua barabara ya shule ya msingi Igoma yenye urefu wa mita 370 na Nyashana mkoani Mwanza ambazo zote zimejengwa kwa mawe.
Alisema sio Mwanza pekee, bali mkoa wowote wenye uwezo wa kujenga barabara kwa kutumia teknolojia mbadala ikiwemo mawe, unapaswa kufanya hivyo ili kuepuka gharama na kuzuingatia uimara.
“Tutajenga barabara nyingi zaidi za mawe kuliko kutegemea lami ambayo tunaagiza nje ya nchi,” alisema.
Meneja wa Tarura wa mkoa huo, Mhandisi Gudluck Mbanga alisema pamoja na uimara wa barabara za mawe, pia ujenzi wake unatengeneza fursa za ajira kwa makundi mbalimbali ya wananchi.
“Kwa kifupi inatusaidia sana kwa sababu Jiji la Mwanza lina miinuko yenye mawe ambapo barabara za gravu zinashindwa kupitika hasa wakati wa mvua,” alifafanua.
Katika Jiji hilo, alibainisha kuna jumla ya kilomita 2,000 za mtandao wa barabara zinazo simamiwa na TARURA, ambapo kati ya hizo mtandao wa barabara za mawe ni kilomita 16 pekee sawa na asilimia 0.2.
Naye Mhandisi wa barabara wilayani Nyamagana, Jane Mdula alisema kwa sehemu kubwa ujenzi wa barabara za mawe unafanywa na watu na sio mitambo.
Alitolea mfano gharama za ujenzi wa barabara ya Igoma yenye urefi wa mita 370 ambayo ujenzi wake unagharimu Sh167 milioni na kwamba imezalisha ajira lukuki za uchongaji mawe kwa wananchi wa kawaida.
Matumizi ya mawe katika ujenzi wa barabara, yameleta fursa ya kipato kwa wafanyakazi katika mgodi wa mawe, alisema Irene Musa mkazi wa Mkoa huo.
Hata hivyo Ibrahim Musa, kijana mwenye umri wa miaka 18 anayefanya kazi kwenye machimbo hayo, ameeleza kuwa kupitia shughuli ya uchongaji wa mawe yanayotumika katika ujenzi wa barabara ameweza kujiingizia kipato ambacho hukitumia kuwasaidia wazazi wake.
Ujenzi wa barabara za mawe unatajwa kuwa ni wagharama nafuu ukilinganisha na ule wa barabara za lami, lakini pia unatoa fursa nyingi za ajira kwa wananchi wenye uwezo wa kushiriki kwenye kazi za ujenzi wa barabara, vilevile unasaidia kufungua barabara na kuwawezesha wananchi kufikia huduma za kijamii kama shule na hospitali kwa urahisi zaidi
No comments:
Post a Comment