SERIKALI YANUNUA UMEME WOTE WA MADOPE-LUDEWA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Sunday 31 July 2022

SERIKALI YANUNUA UMEME WOTE WA MADOPE-LUDEWA





Waziri wa Nishati, Mhe Januari ametoa ufumbuzi wa changamoto ya miaka mingi ya mgawo wa umeme wa masaa 12 kwa vijiji 20 katika Wilaya ya Ludewa ambavyo vimekuwa vikipata umeme kutoka kampuni ya Madope.


Kampuni hiyo ya Madope inayoendesha mradi huo mdogo wa umeme wa maji (MW 1.7 inaundwa na wadau mbalimbali wakiwemo Jumuiya ya Watumia Umeme Lugarawa na Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa.


Changamoto hiyo ya mgawo wa umeme imetokana na waya unaotumika kusambaza umeme kuwa mdogo ukilinganisha na mahitaji ya wananchi ambao wanaotumia umeme kwa shughuli za kiuchumi kama vile kuendesha mashine za kukamulia alizeti na kukoboa na kusaga nafaka.


Akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Lugarawa wilayani humo, Waziri Makamba amesema kuwa, Serikali kupitia TANESCO imeamua kununua umeme wote unaozalishwa na kampuni hiyo baada ya kufanya mazungumzo na wadau wote wanaohusika na mradi huo pamoja na TANESCO.


Amesema kuwa, kwa TANESCO kununua umeme huo kutawezesha wananchi kupata umeme wa uhakika kwani kwa sasa katika megawati 1.7 zinazozalishwa, umeme unaotumika ni 0.3 na pia kampuni hiyo ya Madope itapata mapato.


Ameongeza kuwa, Wataalam wa TANESCO watafika Lugarawa tarehe 7 Agosti 2022 ili kufanya tathmini ya Miundombinu ya Usafirishaji umeme pamoja na kusaini mikataba ya makubaliano hayo na inategemewa kuwa ifikapo mwezi wa Pili mwaka 2023 wananchi hao watakuwa wameshaanza kupata umeme wa uhakika.


Mradi huo wenye wateja 3200 kwa sasa umeleta manufaa mbalimbali kwa wananchi wa Kijiji hicho ikiwemo kutoa huduma ya umeme katika vituo vya afya, shule za Sekondari 5, shule za msingi 19 na kituo kimoja cha kulelea watoto yatima.


Utekelezaji wa Mradi wa umeme wa Madope umewezeshwa na wadau mbalimbali ikiwemo Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambao ulitoa shilingi Bilioni 4.5 kuendeleza mradi huo.


Wananchi pamoja na viongozi katika Wilaya hiyo akiwemo Mbunge wa Ludewa,, Mhe. Joseph Kamonga wamemshukuru Waziri wa Nishati kwa kutoa ufumbuzi wa changamoto hiyo ambayo imedumu kwa muda mrefu.


Akiwa wilayani humo Waziri wa Nishati ameendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia ambapo ametoa mitungi ya gesi kwa kinamama ikiwa ni mradi wa majaribio utakaofanyiwa tathmini ili Serikali itengeneze mkakati bora wa kitaifa wa namna bora ya kusambaza nishati hiyo nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso