KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa (2022) Sahili Nyanzabara Geraruma, amezindua Miradi ya Maendeleo pamoja na kuweka mawe ya Msingi katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama.
NA MARCO MADUHU-SHINYANGAPRESSCLUBBLOG
Mwenge wa Uhuru leo Julai 30 upo katika Manispaa ya Kahama, ukitokea Halmashauri ya Msalala, ambapo umetembelea Miradi Mitano yenye thamani ya Sh. bilioni 4.9.
Sahili akizungumza wakati wa ukaguzi wa Miradi hiyo, amesema Miradi yote ni mizuri na na ndiyo maana ameridhia kuizindua na kuweka mawe ya msingi.
"Nimekagua Miradi yote ni mizuri Kahama mmeupiga Mwingi, endeleeni hivyo hivyo kutekeleza Miradi na kuboresha huduma kwa wananchi," amesema Geraruma.
Aidha, awali akizundua mradi wa Majisafi na salama wa Ngongwa-Kitwana ,ambao umetekelezwa kwa ushirikiano wa Mamlaka mbili za Maji, (SHUWASA), (KUWASA) na Wakala wa Maji (RUWASA), amewataka wananchi kuitunza miundombinu hiyo ya Maji ili nayo iwatunze na kuendelea kupata huduma ya Safi.
Pia akiwa katika ujenzi wa Jengo la uchunguzi la Magonjwa katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama, amewapongeza wa ujenzi huo ambao utasaidia wananchi wa Kahama kupata huduma ya matibabu karibu na kuacha kusafiri kwenda Bugando Jijini Mwanza au Mhimbili Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine amewaasa wananchi wa Kahama, kuwa siku ya kuhesabiwa Sensa ya watu na makazi, siku hiyo wajitokeze kwa wingi kuhesabiwa na kutimizia malengo ya Serikali kupata idadi ya watu wake kamili.
Awali Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama Clement Mkusa, amesema Mwenge huo wa Uhuru katika Manispaa hiyo utakimbizwa Kilomita 105 na kupitia Miradi Mitano ya maendeleo, yenye thamani ya Sh.bilioni 4.9.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kahama Festo Kiswaga ametaja Miradi hiyo Mitano ya Maendeleo ambayo imepitiwa na Mwenge huo wa Uhuru, kuwa ni uzinduzi wa Mradi wa Maji, kuweka Mawe ya Msingi katika jengo la uchunguzi la magonjwa,mradi wa Taka Ngumu, pamoja na Bweni la watoto wenye ulemavu katika Shule ya Msingi Mwime.
Aidha, Mwenge huo wa Uhuru kesho utakimbizwa katika Halmashauri ya Ushetu na baada ya hapo utakabidhiwa katika Mkoa wa Tabora.
Kauli Mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka huu (2022) inasema "Sensa ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo, Shiriki kuhesabiwa kwa Maendeleo ya Taifa.
No comments:
Post a Comment