Mshtakiwa namba moja katika kesi namba 10/2022, Diana Bundala maarufu Mfalme Zumaridi amemkataa hakimu anayesikiliza kesi yake, Monica Ndyekobora kwa kile alochodai kukosa imani naye.
Ombi la kumkataa hakimu huyo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, limewasilishwa leo Julai 11, 2022 na Steven Kitale, wakili wa Mfalme Zumaridi wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya kuendelea kusikiliza ushahidi.
Katika kesi hiyo Mfalme Zumaridi na wenzake nane wanakabiliwa na shtaka la kushambulia na kumsababishia majeraha Ofisa wa Jeshi la Polisi na kumzuia Ofisa Ustawi wa Jamii kutekeleza majukumu yake.
Bila kuweka wazi sababu za mteja wake kutokuwa na imani na hakimu, Kitale amesema upande huo wa utetezi unasubiria maamuzi ya hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Monica Ndyekobora kuhusu hoja zilizowasilishwa na mshtakiwa mezani kwake (chemba).
Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Emmanuel Luvinga ameiambia mahakama kwamba kesi hiyo imeitwa leo kwa ajili ya kusikiliza ushahidi huku upande huo ukiwa umeleta mashahidi wawili kwa ajili ya kutoa ushahidi katika kesi hiyo.
Luvinga ambaye aliambatana na wakili, Deogratius Lumanyika amewataja mashahidi hao kuwa ni Askari wa Jeshi la Polisi, WP4592 Sajenti Paulina na F1468 Sajenti Joanes Mlashani.
Somazaidi:https://www.mwananchi.co.tz/mw/habari/kitaifa/mfalme-zumaridi-amkataa-hakimu--3876116
No comments:
Post a Comment