NA MWANDISHI WETU-THRDC
Meneja Programu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Bi. Remmy Lema akiambatana na Afisa mkuu wa dawati la wanachama, Bi. Lisa Kagaruki wametembelea shirika la uratibu wa kanda ya nyanda za juu kusini, Paralegal Primary Justice (PPJ) lililopo katika halmashauri ya wilaya ya Kyela, mkoani Mbeya.
PPJ ilianzishwa mwaka 2012 n kusajiliwa rasmi mwaka 2013 na kufanya kazi za utoaji wa msaada wa kisheria, katika utetezi wa haki za watoto na wanawake ambao hukumbana na changamoto hasa kwenye maswala ya umiliki wa ardhi unaosababishwa na mfumo dume.
PPJ inawawezesha vijana wa kata ya Busokelo kuelewa na kushiriki katika utekelezaji wa sera za umma na kushiriki katika kamati za halmashauri pamoja na matumizi ya fungu la vijana (4%) linalotolewa na halmashauri ili kuwawezesha vijana kuwa na uwezo wa kujitegemea kiuchumi. Katika eneo hili taasisi imefanikiwa kufikia jumla ya vijana 980 kupitia vikundi 57 vya uwezeshaji kiuchumi ambapo vilivyoundwa na taasisi ili kuwawezesha vijana hao kujitegemea kiuchumi, katika kata ya Busekelo.
PPJ inashirikiana na madawati ya jinsia pamoja na ofisi ya ustawi wa jamii katika usuluhishi wa migogoro ya familia, ambapo kwa mwaka 2021-2022 pekee imefanikiwa kusuluhisha jumla ya kesi 28, 5 kati yao ni kesi za wajane.
PPJ imekuwa ikisaidia taasisi zingine kubwa kama ADP- Mbozi na IRDO katika utambuzi wa watoto waishio katika mazingira magumu, ambapo mpaka sasa taasisi imesaidia kaya 48 zenye watoto 49 (30 Ke) na (19 Me) waathirika wa VVU kupatiwa usaidizi wa mahitaji mbali mbali hasa maswala ya elimu.
Mkurugenzi wa PPJ, Bw. Gabriel John anaushukuru Mtandao kwa kuwa na utaratibu wa kutoa mafunzo kwa wanachama wake ambayo yamekuwa yakiwajenga kuwa na ujasiri wa utekelezaji wa kazi zake katika maeneo walipo bila woga.
PPJ inakiri kukumbana na changamoto kadhaa ikiwemo;
1)Uchache wa rasilimali fedha kuiwezesha taasisi kufikia jamii kwa ukubwa zaidi, ambapo mpaka sasa jamii kubwa iliyofikiwa na taasisi ni katika eneo la Busokelo pekee.
2) Wahanga kuharibu kesi kabla ya kufika PPJ, huwa tayari wamejaribu maeneo mbali mbali na nyingine hufika hadi mahakamani, na hivyo kuipatia mzigo taasisi kufanya utatuzi.
3)Rushwa inayopelekea baadhi ya kesi kuishia polisi, hii inatokana na baadhi ya wazazi kumalizia kesi baina yao, polisi na watuhumiwa bila kujali haki za muathirika.
Meneja programu wa mtandao wa Watetezi wa haki za binadamu Tanzania, Bw. Remmy Lema ameipongeza PPJ kwa kazi nzuri inazofanya, lakini pia ameeleza kuwa mtandao unafanya kazi kuhakikisha unawajengea uwezo wanachama wake katika eneo la uandishi wa miradi na maandiko mbali mbali yatakayoiwezesha taasisi kupata rasilimali fedha kutoka kwa wafadhili lakini pia kupata mafunzo yatakayowapatia ujuzi na mbinu mbali mbali za utekelezaji wa miradi pindi itakapopatikana ili waweze kufanya kazi zao kuhakikisha jamii inanufaika na kazi zao.
No comments:
Post a Comment