Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan leo Juni 06/2022 ameshuhudia utiaji saini wa mikataba ya miradi ya maji katika miji 28, hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
Rais Samia ameipongeza Wizara ya Maji kwa kusimamia miradi ya maji inayotekelezwa nchini huku akiwataka kuongeza jitihada katika kusimamia miradi hiyo mipya katika miji 28.
"Wizara ya Maji mmebadilika sana, mlinipa tabu mwanzo tulielezana ukweli mambo ya kudesign mamiradi mikubwa kuliko yanayotakiwa, lakini tumeelezana ukweli mpo kwenye mstari sasa mnakwenda vizuri" ameeleza Rais Samia
Rais Samia ameeleza kuwa Miradi hiyo mipya iliyosainiwa ni matokeo ya ushirikiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na India
"Mradi huu ambao leo tunasaini ni matokeo ya ushirikiano mzuri uliopo baina ya serikali yetu na India ambao wametupa mkopo wa Dola milioni 500, fedha hizi zitafanya kazi Bara kwa kiasi kikubwa na kiasi kidogo kitaenda Zanzibar"
"India wamekuwa wakituunga mkono kwenye mambo mengi, tuna uhusiano mzuri wa kibiashara, biashara zetu zimepanda mpaka kufikia dola bilioni 4" ameeleza Rais Samia
Katika hatua nyingine Rais Samia ameeleza kuwa serikali yake itaendelea kujenga na kusimamia miradi ya maji ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya CCM
"Serikali itaendelea kujenga miradi ya maji katika kila eneo la nchi yetu ili kutimiza utekelezaji wa ilani ya CCM ili kuhakikisha ifikapo 2025 huduma ya maji safi inafikia asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini" amesema Rais Samia katika hafla hiyo
No comments:
Post a Comment