MTOTO MWENYE UGONJWA WA KIFAFA APIGWA, AUNGUZWA MOTO MGUUNI NA KUTISHIWA KUFUKUZWA NA MAMA WA KAMBO-KAHAMA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday, 25 June 2022

MTOTO MWENYE UGONJWA WA KIFAFA APIGWA, AUNGUZWA MOTO MGUUNI NA KUTISHIWA KUFUKUZWA NA MAMA WA KAMBO-KAHAMA

 


NA PASCHAL MALULU-HUHESO BLOG


Shirika la kutetea haki za binadamu (SHIHABI) Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga limelaani tukio la ukatili wa mtoto wa kiume mwenye umri kati ya miaka 10-11 kupigwa na kuunguzwa na moto na mama yake wa Kambo Mtaa wa Nyihogo Kata ya Nyihogo wilayani humo.

 

Akizungumza na Huheso fm eneo la tukio mwenyekiti wa Shina namba tano ambaye pia ni kiongozi wa shirika hilo Solomon Juma amesema tukio hilo limetokea Juni 25,2022 majira ya asubuhi na wanalaani kwa nguvu zote kwani kitendo hicho kilichofanywa na mama huyo ni ukatili ambao hauwezi kuvumiliwa.

 

Amesema mtoto huyo ni mgonjwa ambaye huwa anaanguka (Kifafa) hivyo anakosa usaidizi wa malezi ya kutosha na mtoto amejeruhiwa sehemu za Jicho, mguuni kwa kuchomwa na moto hivyo wanaiomba serikali kumnusuru mtoto huyo.

 


Wakizungumza baadhi ya wananchi na wakazi wa eneo hilo ambao wameshuhudia tukio hilo wamesema mama huyo ajulikanae kwa jina la Amina (Mama Sam) amekuwa akimpiga mtoto huyo mara kwa mara na kushindwa kumhudumia ipasavyo kama mlezi wake.

 

Mmoja wao aitwaye Mama Rama amesema serikali inapaswa kuwaajibisha wazazi hao akiwemo baba wa mtoto kwani kwa kitendo alichokifanya mama huyo wa kambo wa mtoto ni ukatili ambao haupaswi kufumbiwa macho kwani mtoto huyo amekuwa hata nguo zake akijifulia.

 

Amesema mama huyo amekuwa na tabia ya kumtishia mtoto huyo kumuua kwa kipigo ambapo siku ya jana Juni 24, alimpiga na kuanza kumfukuza na wameiomba serikali kumchukua mtoto huyo kwenda kulelewa na serikali kwenye vituo vya kuhudumia watoto wenye uhitaji.

 


Kwa upande wake kamanda wa Sungusungu wa shina namba tano, Anton Chiza amesema baada ya kufika kwa mama huyo alimhoji na alikana kuhusu kumpiga mtoto huyo na kumuunguza moto na alipomuuliza mtoto alikiri kuwa mama huyo amekuwa akimpiga na kumchoma moto.

 

Hata hivyo serikali ya eneo hilo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi limemkamata mama huyo kwa hatua Zaidi za kisheria.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso