Akizungumza muda mfupi baada ya kuzindua mradi huo uliotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh15.7 bilioni, Rais Samia ameagiza fedha hizo zirejeshwe kutokana na fedha za kuunganishiwa huduma zitakazolipwa na wananchi.
“Fedha hizi ni mkopo utakaorejeshwa kupitia fedha wanazolipa watu wanaounganishiwa huduma, na zitahamishwa katka mamlaka moja hadi nyingine kuharakisha kazi ya kuwaunganishia wananchi huduma,” amesema Rais Samia
Huku akielezea kuridhishwa na kazi inayofanywa na Wizara ya Maji katika utekelezaji wa miradi ya maji sehemu mbalimbali nchini, Rais Samia amewataka wakazi wa Wilaya ya Missenyi watakaonufaika na mradi huo kutunza miundombinu yake pamoja na mto Kagera ambao ndio chanzo cha maji kuwezesha huduma hiyo kuwa endelevu.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Anthony Sanga amesema zaidi ya lita za ujazo milioni 8 za maji zitazalishwa kwa siku kulinganisha na mahitaji halisi ya lita za ujazo milioni 5, hali inayofanya mradi huo kuwa na ziada ya lita za ujazo milioni 3.
Kwa sasa, mradi huo utahudumia watu zaidi ya 35,000, ingawa uwezo halisi ni kuhudumia zaidi ya watu 65,000, hali inayomaanisha kuwa mradi huo utakuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi bila kuwepo upungufu wa maji.
Rais Samia anayeendelea na ziara yake ya siku tatu mkoani Kagera anatarajiwa kuhutubia wananchi katika mkutano wa hadhara unaotarajiwa kufanyika uwanja Kaitaba mjini Bukoba.
No comments:
Post a Comment