Na Patrick Mabula , Kahama.
Afisa usalama wa shirika la umeme (Tanesco ) wa kanda ya Magaharibi, Said Songwe amesema Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga kuwa inaongoza katika matukio ya wizi wa miundombinu ya umeme hali iliyopelekea shirika kupata hasara zaidi shilingi milioni 400.
Akiongea mbele ya mkuu wa Wilaya ya Kahama, Festo Kiswaga aliyekuwa ameitisha kikao cha pamoja cha viongozi wa Sungusungu na Tanesco hivi karibuni katika kupanga mkakati wa ulinzi wa miundombinu hiyo amesema matukio hayo yamekithiri wilayani hapa.
Songwe amesema katika mikoa ya kanda ya magaharibi Kahama imekithiri katika matukio ya wizi wa miundombinu ambayo ni waya na mafuta kwenye trasfoma zake hali inayolitia hasara shirika pamoja na watu kukosa huduma umeme.
Meneja wa Tanesco wa mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Grace Ntungi amesema wezi hao hukata nyaya za usalama zinazofungwa kwenye trasfoma, kuiba mafuta na hadi sasa zaidi ya trasfoma 40 zimeharibika na kulisababishia hasara shirika zaidi ya sh.400 milioni pamoja na wateja kukosa huduma.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Festo Kiswaga amesema amefanya mkutano huo kwa lengo la kuwataka walinzi wa jadi Sungusungu kujipanga kulinda miundombinu ya umeme iliyopo katika maeneo yao kama sehemu ya wajibu wao wa ulinzi na kukomesha wizi huo katika maeneo yao.
Kiswaga amesema suala hilo ni baya sana ni uhujumu uchumi na kuwataka Sungusungu kwa kushirikiana Tanesco na vyombo vingine vya ulinzi lipo mikononi mwao kulinda miunndombinu iliyopo katika maeneo yao na watakaofanikiwa kukamata wezi au kuwafichua wakamatwe watapewa sh.500,000 na cheti maalumu.
Kwa upande wake kiongozi wa Sungusungu wa wilaya ya Kahama , mtemi Bunzali Kashindye alisema ameyapokea maelekezo hayo na kuwataka viongozi wa walinzi hao kuanzia vitongoji, vijiji na kata kujipanga kulinda miundombinu ya umeme iweze kuwa salama.
Viongozi wa Sungusungu wa Wilaya ya Kahama wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Kahama alipokuwa akiwapa maelekezo kuilinda miundombinu ya Tanesco kutokana na wimbi la wezi ambao wamekuwa wakiiba nyaya za usalama wa transfoma pamoja na mafuta hadi sasa transfoma 40 zimeharibika kutokana na na wizi huo.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama Ndugu Festo Kiswaga katikati akiwa na viongozi wa Shirika la Tanesco toka kushoto ni Afisa Usalama wa Shirika la Tanesco Said Songwe, Anayefuata meneja wa Tanesco Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Grace Ntungi na kutoka Kulia wa kwanza ni Mtemi wa Sungusungu wa Wilaya Bunzali kashindye na wa pili Timoth Ndanhya katika kikao cha kuwakamata wezi wa miundombinu ya Umeme.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment