Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema hadi kufikia Aprili 2022, deni la Serikali lilikuwa Sh69.44 trilioni ikilinganishwa na Sh60.72 trilioni kwa kipindi kama hicho mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 14.4.Kati ya kiasi hicho, deni la nje lilikuwa Sh47.07 trilioni na deni la ndani lilikuwa Sh22.37 trilioni.
Dk Nchemba amesema hayo leo Jumanne Juni 14, 2022 wakati akiwasilisha hali ya uchumi wa Taifa na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Amesema ongezeko la deni la Serikali lilitokana na kupokelewa kwa mikopo mipya kutoka vyanzo vyenye masharti nafuu na ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.
Aidha, ongezeko la deni lilitokana na kutolewa kwa hatifungani maalumu yenye thamani ya Sh2.18 trilioni kwa ajili ya deni la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) lililotokana na michango ya watumishi wa kabla ya mwaka 1999.
Amesema taarifa ya tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Novemba 2021 inaonesha kuwa deni la Serikali bado ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu kwa kuzingatia ukomo wa viashiria vyote vinavyokubalika kimataifa.
No comments:
Post a Comment