MAMLAKA ya Majisafi na usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA,) imemkamata mteja wao katika eneo la majengo mapya Manispaa ya Shinyanga kwa madai ya kuwaibia maji.
Tukio hilo limetokea June 11, 2022, wakati Maafisa wa Mamlaka ya Maji (SHUWASA) walipofika eneo hilo na kukuta baadhi ya mabomba yamechepushwa hayapo kwenye mfumo wa dira za maji (Mita).
Kaimu Afisa Uhusiano na Umma wa Mamlaka hiyo ya Maji Shinyanga (SHUWASA) Masaka Kambesha, amesema kutokana na huduma anayotoa mteja huyo na bili zake za maji zinatoka ni tofauti, ndipo wakafanya kutembelea eneo lake, na kukutana na wizi wa maji kwa baadhi ya mabomba kuchepushwa hayapo kwenye usomaji wa mita.
“Tupo hapa kwa mteja wetu wa maji, tumeamua kumtembelea ili kujihakikisha kama bili zake za maji zina uhalisia na matumizi yake, lakini tumefika hapa tumebaini anatuibia maji,”amesema Kambesha.
“Baadhi ya mabomba kama unavyoona Mwandishi wa habari yamechepushwa hayapo kwenye mfumo wa dira za maji (Mita) hivyo wanatumia maji bure,”anaongeza.
Aidha, Mwanasheria wa Mamlaka hiyo Happy Richard, amesema mteja huyo amekiuka Sheria ya Majisafi na usafi wa mazingira Namba 5 ya mwaka 2019 hivyo wanakwenda kumchukulia hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria hiyo ikiwamo na kumtoza faini.
Kwa upande wake mhusika wa tuhuma za kuiba maji ambaye aliomba jina lake lihifadhiwa kwa sababu za kibiashara, amesema hata yeye ameshanghaa kuona mifumo hiyo ya mabomba kuchepushwa na kudai kuwa huenda kazi hiyo imefanywa na fundi wake bila ya yeye kujua.
No comments:
Post a Comment