Wananchi wa kijiji cha Rau River Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wamefunga ofisi ya kijiji hicho wakidai wanashinikiza kufanyika mikutano ya kijiji pamoja na kusomewa mapato na matumizi ya mashamba ya mpunga ya kijiji hicho ambayo hawajasomewa kwa miaka saba.
Wananchi hao wamebandika mabango katika ofisi hiyo ya kijiji, yenye jumbe mbalimbali ikiwamo ya kutaka mtendaji na mwenyekiti wa kijiji waondolewe.
Wamedai kuwa wanashinikiza viongozi hao kuondolewa kutokana na ubadhilifu wa Sh.19 milioni ambazo matumizi yake hayajulikani.
Wakizungumza leo Jumatatu Mei 9, 2022 wamedai kuwa mkutano wa mwisho kuitishwa kijijini hapo ni mwaka 2015 ambao ulivurugika baada ya wananchi kuhoji fedha zitokanazo na mashamba ya kijiji ya mpunga.
Baadhi ya mabango yaliyowekwa kwenye ofisi ya kijiji cha Rau River Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro baada ya ofisi hiyo kufungwa.
Mkazi wa kijiji hicho, Elenati Muhamed amesema kero ya wananchi wa kijiji hicho ni kutokuwepo mkutano wa kijiji pamoja na kutojua mapato na matumizi ya mashamba ya mpunga kwa miaka saba sasa.
Amesema mkutano wa mwisho ulifanyika tangu mwaka 2015 na kubainika upotevu wa zaidi ya Sh8 milioni na kwamba hadi sasa hakujawahi kufanyika tena mkutano wa kijiji.
Kwa upande wake Muhamed Massawa amesema kijiji kina mashamba 47 ya mpunga maarufu kama maboda ambayo ni ya kijiji ambayo hukodishwa kwa Sh400,000 kwa boda moja kwa kila msimu wa kilimo na kwamba kwa mwaka hukodishwa kwa misimu mitatu.
Amesema kijiji kina maboda 942 ambayo ushuru ni Sh4,000 kwa kila boda la mpunga huku block ziko 9 ambazo hutozwa Sh150,000/ kwa kila block, ambao ni ushuru wa kuvuna huingizwa kwenye mapato ya kijiji.
Baadhi ya mabango yaliyowekwa kwenye ofisi ya kijiji cha Rau River Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro baada ya ofisi hiyo kufungwa.
“Kijiji chetu kina mapato mengi yanayotokana na mashamba ya mpunga lakini wananchi hatujui yanaenda wapi tunaomba mkuu wa mkuoa aingilia kati swala hilo hili kumaliza mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu” amesema
Kwa upande wake mwenyekiti Kijiji hicho, Elibariki Molla amekiri kufungwa kwa ofisi hiyo na kwamba akisema kuwa imefungwa na baadhi wananchi ambao hawataki maendeleo ya kijiji.
"Mgogoro huu upo kwa mkuu wa wilaya na unashughulikiwa huko hivyo wanatakiwa kuwa na subira na uamuzi mzuri utatoka kwa Mkuu wa Wilaya ambako ndiko walipeleka barua za malalamiko" amesema
Mtendaji wa kijiji cha Rau River, Mary Kundya amesema hana taarifa za kufungwa kwa ofisi na yuko nyumbani kwa matatizo ya kiafya.
Diwani wa Kata ya Kahe Magharibi, Aloyce Mumburi amesema malalamkiko ya wananchi ni ya kweli na kwamba kijiji hicho hakijawahi kufanya mikutano ya kijiji kwa muda mrefu na kuwataka wenyeviti wa vijiji kufutata taratibu na sheria za kuongoza wananchi.
"Kimsingi watendaji washauri vyema wenyeviti wa vijiji kuhusu swala la kiserikali la uitishwaji wa mikutano ya kijiji pia Mkurugenzi mtendaji kuandaa semina elekezi kwa wenyeviti wa vijiji ili waweze kutimiza majukumu yao na kuondokana na migogoro ya wananchi" amesema
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Moshi, Kastory Msigala amesema wananchi kufunga ofisi ni kosa kisheria kwa kuwa wapo baadhi ya wananchi wanahitaji huduma na kwamba anafuatilia kujua sababu iliyopelekea hadi wafikie uamuzi huo.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment