WADAU WA MAENDELEO WAOMBWA KUCHANGIA SENSA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Sunday, 8 May 2022

WADAU WA MAENDELEO WAOMBWA KUCHANGIA SENSA


Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ametoa wito kwa washirika wa maendeleo kuchangia kwa hali na mali kiasi cha dola milioni 80 za Marekani kwa ajili ya kufanikisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linayotarajiwa kufanyika tarehe 23 Agosti mwaka huu.




Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza na Washirika wa Maendeleo wakiwemo Mabalozi wakati wa mkutano wa majadiliano ya uchangiaji wa bajeti ya zoezi la sensa linalotarajiwa kufanyika tarehe 23 Agosti 2022, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.


Dkt. Nchemba ametoa wito huo jijini Dar es Salaam alipofungua mkutano wa washirika wa Maendeleo wakiwemo Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.

Alisema kuwa Sensa ya watu na Makazi imekadiriwa kugharimu dola za Marekani milioni 272.7 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 626.9 kwa kipindi cha miaka 5 kuanzia mwaka 2021/22 hadi mwaka 2025/26 ambapo kati ya fedha hizo serikali itachangia asilimia 70 na kiasi kingine cha dola milioni 81.8 kitachangiwa na washirika wa maendeleo.

Dkt. Nchemba alisema kuwa Sensa ya watu na makazi inatumia rasilimali kubwa ndiyo maana Serikali imeamua kuwashirikisha kikamilifu wadau wa maendeleo na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa siku ya Sensa itakayofanyika tarehe 23 Agosti, 2022.

“Sensa ni muhimu kwa wananchi wote kwa sababu imebainika kuwa wakati wa sensa watu hawajitokezi lakini wanapodai kujengewa miundombinu kama elimu, afya na kutaka maeneo yao kupandishwa hadhi wanajitokeza kwa wingi,lakini tukirudi kwenye takwimu tunakuta idadi ya wananchi wachache” alisema Dkt. Nchemba

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohamed, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Fedha na Mipango, Zanzibar Dkt. Saada Mkuya Salum, aliwashukuru Washirika wa maendeleo kwa kutoa ahadi zao za kusaidia zoezi la sensa na kuwaomba watimize ahadi hizo kwani muda uliobaki ni mfupi.

Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa walioshiriki Mkutano huo wameipongeza Tanzania kwa kufanikisha maandalizi ya zoezi la Sensa kwa kutumia fedha zake za ndani na kutoka kwa baadhi ya Mashirika ya Kimataifa na kuahidi kuwa watachangia vifaa na fedha ili kusaidia kazi hiyo.

Kwa upande wa Benki ya Dunia imeahidi kutoa dola milioni 19 za Marekani kwa ajili ya kuchangia zoezi hilo la Sensa, aidha Shirika la Umoja wa Mataifa (UNWomen) limeahidi kuchangia vishikwambi (kompyuta ndogo) 200 huku mataifa mengine yakiendelea kutoa ahadi za kufanikisha zoezi hilo la Sensa.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa mataifa linalojihusisha na masuala ya Idadi ya Watu na Makazi Bw. Mark Bryan Shreiner, Kamisaa wa Sensa Tanzania Bara Spika Mstaafu Mhe. Anne Makinda, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Bw. Hamza Hassan Juma, na Kamisaa wa Sensa Zanzibar Balozi Mohammed Haji Hamza.

CHANZO: EATV NEWS

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso