Mkurugenzi wa halmashauri ya Biharamulo, Inocent Mkandara, akimkaribisha kamishna wa Ushirikishwaji jamii polisi makao makuu, Dk. Mussa Ali Mussa.
Na Daniel Limbe, Biharamulo
WIMBI la watoto wanaofanya uhalifu kwenye kata ya Kalenge wilayani Biharamulo mkoani Kagera limedaiwa kutishia maisha ya wananchi kutokana na kutochukuliwa hatua kali za kisheria.
Kuibuka kwa kundi hilo, kumejiri ikiwa ni siku chache tangu kuripotiwa uwepo wa vijana wanaojihusisha na uhalifu wa kutumia silaha baridi jijini Dar es salaam huku jeshi la polisi likionya na kuahidi kuwakamata ili sheria ichukue mkondo wake.
Diwani wa kata ya Kalenge, Erick Method, ameyasema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya kata yake kwenye Baraza la madiwani wa halmashauri hiyo ambapo amesema licha ya jitihada za wananchi kuwakamata watoto hao jeshi la polisi limeshindwa kuwafikisha mahakamani kwa madai kuwa wana umri chini ya miaka 18.
Awali akitoa elimu ya ulinzi shirikishi kwa madiwani, watendaji wa kata, vijiji, wenye viti wa vijiji na vitongoji, kamishna wa ushirikishwaji jamii polisi makao makuu, Dk. Mussa Ali Mussa, amesema uharifu hauwezi kwisha nchini iwapo jamii haitakuwa tayari kushirikiana na jeshi la polisi.
Amesema uhalifu umekuwa ukitamalaki kwenye jamii kutokana na kamati za ulinzi na usalama ngazi ya kata kushindwa kutimiza wajibu wao na kwamba kuna kila sababu kwa kutenga bajeti kwaajili ya ulinzi na usalama badala la kujikita kwenye miradi ya maendeleo pekee.
Kwa upande wake, kamishna mwandamizi wa polisi, Engelbert Kiondo,amesema suala la vijana na watoto waharifu (panya road) halipaswi kulaumiana badala yake kila mwananchi anapaswa kutimiza wajibu wake katika malezi na makuzi ya watoto.
Aidha ametumia fursa hiyo kuwataka madiwani kuwahamasisha wananchi na wafanyabiashara kuchangia miradi ya polisi ikiwemo ujenzi wa vituo vya polisi kwa lengo la kudhibiti uharifu kabla na baada ya kutokea.
Licha ya kupongeza mpango wa polisi kata, Diwani wa kata ya Biharamulo mjini, David Mwenenkundwa, amedai uwepo wa askari hao utasaidia kupunguza matukio ya kiharifu na kwamba utaongeza mahusiano ya kuoana na kuoleana.
No comments:
Post a Comment