Nyati mweupe ameonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na kuwa kivutio kwa watalii wa ndani na nje ya nchi wakitaka kumuona.
Nyati huyo ambaye kwa mara ya kwanza ameonekana jana Jumatatu Mei 16, 2022 jioni ndani ya hifadhi hiyo amesababisha watalii wengi waliokuwa hifadhini kuanza kumfatilia na kuanza kuvutia watafiti katika eneo hilo.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Pascal Shelutete amesema nyati huyo ameonekana kwa mara ya kwanza jana na amekuwa kivutio kwa wengi.
Amesema uchunguzi wa awali unaonyesha huenda nyati huyo ni albino sawa na wanyama wengine weupe waliowahi kuonekana katika hifadhi hiyo akiwemo twiga.
"Tutaendelea kumfatilia na kumtunza nyati huyo kwani tangu habari zake zimejulikana kuna wengi wameanza kufatilia" amesema Shelutete.
Hifadhi ya Tarangire iko kanda ya kaskazini kusini mwa Ziwa Manyara.
No comments:
Post a Comment