Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameliagiza Jeshi la Uhamiaji mkoani Mwanza kuchukua hati za kusafiria za wakandarasi wanaojenga meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu kutokana na kushindwa kutekeleza matakwa ya mkataba.
Majaliwa ametoa agizo hilo leo Jumamosi Mei 7, 2022 alipotembelea na kukagua ujenzi wa meli hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo unaotekelezwa kwa gharama ya Sh97.5 bilioni.
Majaliwa ametoa maagizo hayo baada ya kubaini kwamba Kampuni ya GasenTec Ship-Building engineering ya nchini Korea imelipwa fedha asilimia 80 huku ujenzi huo ukiwa asilimia 65 pekee.
Amesema kwa mujibu wa mkataba ujenzi wa meli hiyo hadi kufikia leo Mei 7, 2022 ulitakiwa uwe umefikia asilimia 95.
"Nimeingia ndani kukagua nimepata taarifa, lakini yako mambo sijardhishwa nayo. Kwanza nimepata taarifa kwamba kampuni inayojenga meli hii imeuza hisa kwa kampuni nyingine bila serikali kujua.
“Pia ndani kuna fukuto la mabishano, watumishi wa serikali wanasimamia stahiki za serikali wakandarasi nao wanang'ang'ana walipwe fedha zaidi," amesema Majaliwa.
Pia amesema kwamba katika ujenzi wa meli hiyo kulikuwa na wafanyakazi 118 lakini wamefukuzwa na kubaki wafanyakazi 22 ambao hawawezi kukamilisha ujenzi wa meli hiyo.
"Sijui wanatega nini ili waweze kumaliza, naamini Watanzania ni werevu. Walisema Corona tumeongeza muda kutoka miezi 22 hadi miezi 33 lakini hadi muda huu bado," amesema.
Ameongeza; " Nawaagiza Uhamiaji ichukue Passpoti zote za wakandarasi hadi meli ikamilike, nimezungumza na Balozi wa Korea ameridhia, nimewasiliana na Rais naye ameridhia," amesema Majaliwa.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment