Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amewataka wafanyabiashara ndogondogo na wajasiriamali wafanye biashara zao kwa uhakika kwa sababu serikali inataka watimize matamanio yao.
Kauli hiyo ameitoa hii leo Mei 24, 2022, mkoani Arusha akiwa kwenye ziara yake ya siku moja, ambapo amekagua masoko ya Mbauda, Kilombero na Machame na kuzungumza na baadhi ya wamachinga wanaofanya biashara kwenye masoko hayo.
"Serikali hii inawatambua na itasimamia matamanio yenu na mtanufaika kwenye ndoto zenu, mtaji uliowekezwa kwenye vibanda hivi na Jiji ni shilingi bilioni moja na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, akaongeza shilingi milioni 500 ili masoko mengi yajengwe," amesema Waziri Mkuu.
Aidha Waziri Mkuu ameongeza kuwa, "Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan nia yake ni kuwafanya muweze kuwa na maeneo yanayotambulika, kisha mpate kipato rasmi ili nanyi muwe wafanyabiashara wakubwa hapo baadaye, hapa Arusha wako wafanyabiashara maarufu ambao walianza kwa kusafisha viatu lakini leo wanamiliki biashara kubwa kubwa,"
Amewataka wafanyabiashara hao wahakikishe kuwa wanafanya biashara kwenye maeneo yanayotambulika ili waweze kupatikana kwa urahisi na waweze kupata mikopo ya mitaji kama ambavyo Mheshimiwa Rais ameelekeza.
No comments:
Post a Comment