POLISI mkoani Morogoro linamshikilia Semeni Mrisho Issa (49), mkulima na mkazi wa Duthumi, Wilaya ya Morogoro kwa tuhuma za kupatikana na vipande 18 vya meno ya tembo akiwa ameyahifadhi ndani ya kiroba.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Fortunatus Musilimu amesema hayo leo Aprili 14, mwaka huu kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Aprili 8, majira ya saa 10 jioni eneo la Mgeta, Wilaya ya Mvomero .
Musilimu amesema mtuhumiwa hiyo alikamatwa kutokana na kupata taarifa za msiri wao na kumkamata ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, akiwa na meno ya tembo vipande 18, vikiwa ndani ya mfuko wa kiroba ambapo uzito wake ni kilo 61 na thamani yake bado haijafahamika.
Amesema kukamatwa kwa mtuhumia huyo ni ushirikiano kati ya polisi, Jeshi la Uhifadhi la Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, iliyopo chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa).
Kamanda huyo amesema mtuhumiwa alipohojiwa mbele ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyandira, kinachopakana na Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, alikiri kupatikana na meno hayo na kwa siku tofauti aliingia hifadhini kuua Tembo na kuchukua meno hayo na kufahifadhi.
Amesema bado wanaendelea kumhoji na yatakapokamilika mahojiano, atafikishwa mahakamani.
Naye Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, Halid Mngofi amesema , Jeshi la Uhifadhi la Tanapa katika hifadhi hiyo kwa kushirikiana na polisi, wameanza kufanya doria ya pamoja, ili kukabiliana na viashiria vya uhalifu wa ujangili wa wanyama pori.
Amesema vipande wa meno ya tembo vilivyokamatwa ni sawa na tembo watano wameuliwa na inaonesha yalihifadhiwa miaka mitatu nyuma, na mtuhumiwa alikuwa akitafuta soko la meno hayo.
No comments:
Post a Comment