Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Nishati imeagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kuendelea kununua nguzo za umeme kutoka kwa wazawa Kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyokubalika.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba leo Aprili 30, 2022 wilayani Mafinga Mkoani Iringa katika kikao kazi alichokutana
na wadau wa biashara wa nguzo wakiwemo wakulima,wachakataji wauzaji,wamiliki wa viwanda vya nguzo za umeme pamoja na wabunge wa mikoa ya Njombe na Iringa.
Akizungumza na wadau hao Mh Waziri amesema "TANESCO na REA watanunua nguzo zote kutoka Tanzania Kwa kuzingatia viwango vya ubora unaotakiwa"
Aidha amewataka kuanzisha mfumo ambao utawawezesha kuhakiki nguzo ili kupatikana kwa nguzo zenye ubora zitakazoweza kukidhi vigezo vya kuuza nguzo hata nje ya Nchi.
"Sisi tunategemea kwamba kuwe na mfumo wa wadau wa nguzo wa Mikoa yetu hii ya kuhakikisha kwamba tunachungana na kudhibitiana kwenye ubora" amesema Waziri Makamba.
Ameongeza kuwa Serikali iko tayari kugharamia mafunzo kwa wazawa wakajifunze nje ya nchi namna bora ya kuandaa nguzo hizo ili kulinda soko la ndani.
"Serikali inaposema itanunua nguzo kwa wazawa inategemea hamtaiangusha kwa kuzalisha nguzo ambazo zinaubora hili ni muhimu sana" amesisitiza Waziri Makamba.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Maharage Chande amesema TANESCO inatekeleza maagizo ya Serikali kwa kuwapa kipaumbele wazawa katika ununuzi wa nguzo.
"Niwahakikishie TANESCO tunaendelea kuboresha katika masuala ya mfumo wa manunuzi ya nguzo, na huko tunakoelekea kutakuwa na uwazi zaidi wa mchakato mzima niwahakikishie hilo kwa asilimia 100" amesema Maharage.
Ameongeza kuwa TANESCO itakutana na wadau hao mapema wiki ijayo ili kuzungumza kwa kina na kukubaliana nao kwenye masuala ya ubora.
"Kama kuunda chama cha uhakiki wa ubora wa nguzo kianzishwe kama alivyoagiza Mh Waziri na sisi kama Shirika tutatoa ushirikiano, tuangalie jinsi gani ya kufanya tupate bei shindani na nguzo zenye ubora" alimalizia Maharage.
Naye Mkurugenzi Mkuu REA, Mhandisi Hassan Said amesema REA kwa upande wao kama wadau wengine wamepokea agizo la Serikali huku akisisitiza kwa wadau wa nguzo kuzingatia ubora.
Ameongeza kuwa kwa hivi sasa REA haina nguzo ambazo imeagiza nje ya Nchi na hii imesaidia kukuza soko la viwanda vya ndani.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Queen Sendega ameishukuru Serikali kwa kutambua umuhimu wa kukutana na wadau wa nguzo wa mikoa ya Iringa na Njombe kwani asilimia 48 ya mapato ya mkoa wa Iringa yanategemea sana uuzwaji wa mazao ya misitu ikiwemo nguzo.
Ameongeza kwa kuwataka wadau wa nguzo kuongeza uaminifu na kuzingatia ubora unaotakiwa katika soko la ndani ili kuwasaidia kupata soko la nje.
kikao hicho kilihitimishwa Kwa agizo la Mh Waziri Makamba kutaka iundwe kamati ya majadiliano itakayohusisha wadau wote muhimu wa nguzo ikiwemo TANESCO na REA ili kuona namna nzuri ya kutekeleza makubaliano yaliyotokana na kikao hicho.
No comments:
Post a Comment