Zikiwa zimepita siku saba tangu timu ya Simba kushindwa kutinga hatua ya Nusu Fainali ya michuano ya Kombe la Washindi Afrika,na saa chache zikibaki za pambano la Kariakoo Derby dhidi yao na watani zao Yanga,baadhi ya wapenzi na mashabiki wa timu hiyo wametoa ushauri kwa uongozi wa timu hiyo.
Wanazi hao kwa nyakati tofauti wakiongea na simu kutoka sehemu mbalimbali nchini,walitoa ushauri kwa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba kutoachana na Kocha aliyepo, Pablo Franco Martin kwani amedhihirisha ni Mwalimu mzuri kutokana na kuwa na timu muda mfupi lakini ikifanya vizuri.
Pia kushauri kwa Wanachama,Wapenzi na Mashabiki wa Simba kusahau jinamizi la michuano ya Kimataifa msimu huu na kuelekeza akili katika michuano ijayo.
Katibu wa Simba Tawi la Mwendokasi,wilaya ya Kahama,Sixberth Koyo,alidai matokeo waliyopata katika michuano ya Kimataifa Afrika iwe fundisho kwa Bodi kuhakikisha wanaimarisha kikosi ili msimu ujao timu ifike nusu Fainali.
Koyo alisema imekuwa mazoea kwa timu ya Simba kufikia hatua ya robo fainali michuano ya Afrika hivyo kwa mikakati iliyonayo Bodi haina budi kuimarisha kikosi ambacho kitakuwa Cha ushindi kwa michuano ijayo.
Aidha alitoa ushauri kwa Bodi kuhakikisha wanaendelea kumpa nafasi Kocha Pablo Martin,pamoja na kutambua kuwa walimuajiri kwa mkataba wenye malengo ya kutwaa Ubingwa Tanzania Bara,Kombe la TFF na katika michuano ya Kimataifa wafike nusu fainali.
" Pablo ana kitu fulani katika michuano ya mtoano,ndio maana robo fainali hii tumetolewa kwa penalti tofauti na robo fainali zilizopita,"alisema Koyo.
Aidha alisema Kocha huyo anastahili kupewa nafasi na kupewa Uhuru wa kusajili na kuandaa kikosi kwa ajili ya michuano ya msimu ujao,ambapo atajipambanua mfumo wake wa ufundishaji,ambao ndio utamhukumu.
Kwa upande wake Erickson Rwehumbiza kutoka mkoani Manyara,alitoa ushauri kwa Bodi kufanya usajili wenye tija na kuanza maandalizi mapema kufuatia msimu ujao kuwa mfupi unaosababishwa na uwepo wa michuano ya Kombe la Dunia.
Rwehumbiza nae aliiomba bodi kumpa nafasi Kocha Pablo,kutokana na mafanikio aliyoyaonyesha katika michuano ya Kimataifa na hasa kwakuwa kikosi alichonacho hakukisajili na alikikuta katikati,hata hivyo alikibadili na kuwa bora.
" Nashauri Bodi kumpa nafasi Pablo katika usajili wa wachezaji pia wasimkilize katika kuimarisha benchi la ufundi ili kuwa na kikosi Bora msimu ujao,"alisema Rwehumbiza.
Hata hivyo aliishauri Bodi ya Simba kuimarisha benchi la ufundi hasa Kocha wa viungo kwani toka aondoka Zrane,wachezaji wamekuwa wakipata majeraha Sana na kuwa nje kipindi kirefu.
Nao wapenzi wa Simba kutoka Kahama,Fundi Abdul na Habibu Ally waliishauri Bodi ya Simba,kuimarisha benchi la ufundi kwa kumrejesha kikosini Kocha wa viungo Zrane na aliyepo kumpangia majukumu mengine.
Kwa upande wake shabiki wa Simba kutoka Kidatu wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro,Ramadhani Lityawi,alisema Bodi haina budi kuimarisha kikosi kwa kusajili wachezaji wenye viwango vikubwa zaidi.
Lityawi alisema Bodi ya Wakurugenzi wa Simba ipatiwe Ripoti kutoka benchi la Ufundi ambalo anashauri lisivurugwe zaidi ya kumrejesha Zrane,na kuhakikisha wanatekeleza matakwa ya benchi hilo kusudi msimu ujao ifanye vyema zaidi.
No comments:
Post a Comment