Serikali imekiri kuwa na taarifa kuhusu jiwe la rubi lenye uzito wa kilo 2.8 ambalo linatajwa kuwa linatoka Tanzania lakini bado haijathibitika.
Hata hivyo, tayari mmiliki wa jiwe hilo amejulikana kuwa anatoka nchini Marekani katika mji wa Carifonia, na sasa Serikali inafuatilia nyaraka za umiliki wa jiwe hilo tangu awali.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Aprili 21, 2022 bungeni na Naibu Waziri wa Madini, Dk Stephen Kiruswa alipokuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Mkinga, Dustan Kitandula.
Mbunge huyo aliomba kufahamu kuhusu uvumi wa taarifa za mitandao kuwa jiwe hilo kubwa lenye thamani ya fedha nyingi limetoka Tanzania.
Dk Kiruswa amesema Serikali ilipata taarifa za uwapo wa jiwe hilo tangu Aprili 13,2022 na kwamba, lina thamani ya dola 120 milioni za Marekani sawa na Sh240 bilioni za Tanzania.
Na taarifa zinasema litawekwa sokoni ndani ya siku 30 baada ya mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
"Tuliwasiliana na Ubalozi wetu Dubai na katika kufuatilia, imebainika kuwa mmiliki wake anatoka Marekani, sasa tunafuatilia mmiliki wa awali na kama ni mali ya Tanzania tuone namna gani lilisafirishwa hadi kufika huko," amesema Dk Kiruswa.
Hata hivyo, Naibu Waziri huyo amesema haki ya Watanzania haitapotea ikiwa itathibika lilitoka nchini.
No comments:
Post a Comment