Rais Samia Suluhu Hassan ametoa msamaha kwa wafungwa 3, 826 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 58 ya muungano wa Tanzania.
Na Sharon Sauwa - Mwananchi
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumanne Aprili 26, 2022 na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni imeeleza kuwa msamaha huo unaenda sambamba na masharti mbalimbali ikiwa ni pamoja na wafungwa wote kupunguziwa robo ya vifungo vyao baada ya punguzo la kawaida la moja ya tatu linalotolewa chini ya kifungu cha 48(1) cha Sheria ya Magereza.
“Wafungwa hao sharti wawe wametumikia robo ya vifungo vyao na wawe wameingia gerezani kabla ya Februari 26, 2022 isipokuwa walioorodheshwa katika sharti la 2(1-11),” imeeleza taarifa hiyo.
Pia ametaja wafungwa wengine na masharti ya msamaha huu ni kwa wagonjwa wenye magonjwa ya kudumu uliothibitishwa na jopo la waganga chini ya mwenyekiti mganga mkuu wa mkoa au wilaya na wawe wametumikia robo ya vifungo vyao.
Amewataja wafungwa wazee wenye umri wa miaka 70 au zaidi ambao wametumikia robo ya vifungo vyao na wafungwa wa kike walioingia gerezani wakiwa na watoto wanaonyonya, wasionyonya na wajawazito ambao wametumikia robo ya vifungo vyao.
Wengine waliopata msamaha ni wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kifo ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka 30 na kuendelea.
“Wafungwa wanaotumikia kifungo cha maisha gerezani ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka 20 na kuendelea. Wafungwa wanaotumikia adhabu kwa makosa ya kujaribu kuua ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka 10 na kuendelea,”amesema.
Wengine ni wanaotumikia adhabu ya kuua watoto wachanga ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka 15 na kuendelea na wafungwa wanaotumikia adhabu ya makosa ya uhujumu uchumi ambao wamekaa magerezani kuanzia miaka 20 na kuendelea.
Masauni amewataja wengine ni wanaotumikia adhabu ya makosa ya matumizi mabaya ya madaraka yao ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka mitano na kuendelea.
“Wanaotumikia adhabu kwa makosa ya utakatishaji wa fedha ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka 20 na kuendelea na wafungwa wanaotumikia adhabu ya makosa ya rushwa ambao wamekaa magerezani kwa kuanzia miaka 10 na kuendelea”
Wengine ni wafungwa wanaotumikia adhabu kwa makossa ya usafirishaji na madawa ya kulevya ambao wamekaa magerezani kuanzia miaka 20 na kuendelea na wanaotumikia adhabu kwa makossa ya utekaji au wizi wa watoto ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka 10 na kuendelea.
Wafungwa wengine ni wanaotumikia adhabu kwa makossa ya wizi au ubadhirifu wa fedha na mali za umma ambao wamekaa gerezani kuanzia mika 15 na kuendelea.
Hata hivyo, amesema msamaha huo usiwahusishe wafungwa wa madeni na wafungwa wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi za Parole sura ya 400 Sheria ya Huduma kwa Jamii (Sura ya 291) na kanuni za kifungo cha nje.
No comments:
Post a Comment