Katika kuelekea maadhimisho ya Uhuru wa habari duniani,Klabu ya waandishi wa Habari mkoa wa Shinyanga imefanya mdahalo na Jeshi la Polisi,huku waandishi wakiaswa kujenga tabia ya kufika kwenye maeneo ya matukio,pasipo kutegemea kila Jambo likamilishwa na Polisi.
Na Ally Lityawi
Wito huo ulitolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga,George Kyando,katika mdahalo huo uliokuwa na
lengo la kujadiliana namna ya kuimarisha mahusiano mazuri na Jeshi hilo hasa wanapokutana kwenye matukio.
Kamanda Kyando aliwafahamisha waandishi wa habari juu ya changamoto wanayokumbana nayo katika matukio mbalimbali hususani ya ajali kwa kutakiwa kueleza kwa kina juu ya tukio hilo la ajali.
Kyando aliwafafanulia Waandishi wa Habari kuwa Jeshi la Polisi linapofika kwenye eneo la tukio, lengo Ni kukusanya ushahidi na si taarifa kwa ajili ya waandishi wa habari.
" Tunapofika katika tukio huwa hatukusanyi taarifa za habari, bali tunakusanya ushahidi wa tukio, nanyi fikeni eneo la tukio mpate habari kwa kina,"alisema Kamanda Kyando.
Hivyo aliiomba kada hiyo ya habari ambayo Ina umuhimu kubwa katika jamii kuhabarisha,kuelimisha na kuburudisha wabadilike katika utendaji kazi kwa kukusanya taarifa ili kuhabarisha umma.
Awali akifungua Mdahalo huo,Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoani Shinyanga( SPC ), Patrick Mabula, alisema Jeshi la Polisi na waandishi wa habari wanapaswa kuwa na mahusiano mazuri, kwa sababu wanategemeana katika utekelezaji wa majukumu hasa katika matukio ya kiharifu na ajali za barabarani.
Mdahalo huo umefanyika Aprili 28, 2022 kwa kukutanisha maofisa wa Jeshi la Polisi ngazi za juu mkoani Shinyanga, pamoja na waandishi wa habari mkoani humo kwa lengo la kujadili namna ya kuimarisha mahusiano mazuri wanapokutana kwenye matukio.
Ambapo katika mdahalo huo waliadhimia maazimio manne yatakayokuwa muongozo katika kutekeleza majukumu yao na pasipo mifarakano pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama kwa waandishi pindi wanapotekeleza majukumu yao.
No comments:
Post a Comment