Mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite jijini Arusha, Pendael Mollel (47) na wenzake wawili, jana Ijumaa Aprili 29, 2022, wamepandishwa kizimbani na kusomewa shitaka moja la mauaji ya kukusudia.
Mbali ya Mollel, mkazi wa Kiranyi, Arusha, wengine waliosomewa shitaka hilo ni Onesmo Laizer (35), mkazi wa Ngaramtoni wilayani Arumeru, ambaye ni mlinzi wa mfanyabiashara huyo na Deogratias Mollel (35), mkazi wa Sakina , Arusha, ambaye ni mdogo wa mfanyabiashara huyo.
Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Grace Medikenya alidai mbele ya Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Devotha Msofe kuwa, mtuhumiwa Mollel na wenzake hao walimua kwa kukusudia, Stephen Kivuyo (43), Aprili 18 mwaka huu eneo la Burka, Arusha saa 1:45 usiku.
Baada ya kusomewa shitaka hilo, Hakimu Msofe aliwaeleza watuhumiwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza kesi hiyo, kwani kesi ya mauaji itasikilizwa na Mahakama Kuu, hivyo hawatakiwi kujibu chochote na kesi yao iliahirishwa hadi Mei 10, mwaka huu itakapotajwa tena.
No comments:
Post a Comment