Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu linamshikilia mama mmoja anayefahamika kwa jina la Mwamba Thomas (37) Msukuma kwa tuhuma za kumchoma na maji ya mtoto wake India Itito (4) kwenye mikono yake miwili kwa kile kilichodaiwa mtoto huyo kuiba tambi ambazo ziliandaliwa kwa ajili ya chakula cha mchana.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani humo, ACP Shadrack Masija, imeeleza kuwa tukio hilo la kikatili limetokea Aprili 22, 2022 majira ya saa 10:00 jioni katika Mtaa wa Kidinda, Kata ya Bariadi, Tarafa ya Ntuzu, wilayani Bariadi mkoani Simiyu.
Kaimu kamanda huyo amesema kuwa mama huyo wanaendelea kumshikilia mpaka sasa, wakati upelelezi wa tukio hilo ukiendelea na mara baada ya kukamilika watamfikisha katika vyombo vya sheria.
“Kwa sasa mtoto amelazwa Hospatali ya Wilaya ya Bariadi na anaendelea na matibabu, mara baada kukamilisha upelelezi wa shauri hilo jalada litafikishwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Simiyu kwa hatua za kisheria zaidi,” alisema Masija.
Jeshi hilo limetoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Simiyu kuacha mara moja vitendo vya kujichukulia sheria mkononi ambavyo vinapelekea ukatili dhidi ya watoto na jamii inayo kwa ujumla.
Ni vyema mtoto anapokuwa amefanya makosa akapewa elimu na kuonywa kwa kumpa adhabu ya kawaida tu na si kuwapa adhabu zinazopelekea madhara makubwa.
Katika hatua nyingine jeshi hilo linawashikiria watu wawili Ntengwa Mwanangwa (25) Msukuma, Mkulima Mkazi wa Kijiji cha Ipililo na John Didi (18) Msukuma, Mkulima Mkazi wa Kijiji cha Ipililo WilayanI Maswa kwa kosa la kukutwa wakiwa na Noti 11 Bandia zenye thamani ya Sh. 95,000.
Watuhumiwa hao walikamatwa mnamo Aprili 22, majira ya saa 08:30 mchana wakiwa na noti 8 za Tsh 10,000/= zenye namba zinazofanana na noti tatu za Sh 5,000/= ambazo pia zina namba ambazo zinafanana.
No comments:
Post a Comment