DC Nyamagana awapigia magoti wananchi kuomba washiriki ujenzi shule - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday, 23 April 2022

DC Nyamagana awapigia magoti wananchi kuomba washiriki ujenzi shule


Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi na Diwani wa Kata ya Butimba, Marwa Mkale wamewapigia magoti wakazi wa Kata ya Butimba wakiwaomba kushiriki kikamilifu katika mradi wa ujenzi wa Sekondari ya Nyamagana utakaotekelezwa katika kata ya Butimba mkoani humo.


Ujenzi wa shule hiyo itakayokuwa ikipokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita unatarajia kuanza Mei 2 mwaka huu kwa gharama ya Sh 401 milioni.

Akizungumza jana Aprili 22, 2022 katika uwanja wa shule ya Msingi Iseni 'B' ulipofanyika mkutano huo, Makilagi amesema katika mradi wa ujenzi wa shule hiyo unaofadhiriwa na Mpango wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), wananchi wanatakiwa kutoa mchango wa asilimia 10 mradi huo unapoanza hadi utakapokamilika.

"Mfadhili ameshaweka fedha katika akaunti lakini na sisi tunatakiwa kushiriki kwa namna mbalimbali ikiwemo kwenye uchimbaji wa msingi, kusomba maji na shughuli nyingine tutakazihitajika kufanya, nawaomba jamani wakati utakapofika tujitokeze kutimiza wajibu wetu," amesema Makilagi

Mkurugenzi wa Miradi wa Tasaf nchini, John Stephen amesema mpango huo utaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha maisha na ustawi wa jamii inayoishi katika halmashauri hiyo.

"Mradi huu utakuwa wa miaka mitano, iwapo wakazi wa maeneo unapotekelezwa watatimiza masharti ikiwemo kushiriki kwa asilimia angalau 10, itaongeza ushawishi wa kuleta miradi mingine," amesema Stephen

Diwani wa Kata ya Butimba, Marwa Mkale amesema anaamini wakazi wa kata hiyo watashiriki kikamilifu huku mkazi wa mtaa wa Iseni, Hadija Mussa akisema mbali na kushiriki kufanya kazi pia watajitolea rasilimali fedha pale itakapohitajika.

Katika mradi huo, Tasaf imefadhiri ujenzi wa madarasa matatu yenye ofisi katikati, matundu sita ya choo na bweni litakalokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 120.

Na Mgongo Kaitira - Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso