Viongozi wa bodi na wasimamizi wakuu wa asasi za kiraia 36 kutoka asasi 5 nchini Tanzania wamepewa mafunzo jijini Arusha kuhusu utawala na uongozi bora ili kuweza kutekeleza miradi ya PEPFAR na kuimarisha usimamizi wa mashirika yao.
Hili ni hitimisho la mafunzo haya kwa meneja mradi, wasimamizi wa fedha na wajumbe wakuu wa bodi 108 kutoka asasi za kiraia 18 katika mikoa ya Arusha, Dar es salaam, Dodoma, Iringa, Kilimanjaro, Morogoro, Njombe, Ruvuma na Shinyanga.
Mafunzo haya yameandaliwa na FHI 360 kupitia mradi wa EpiC kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) pamoja na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).
Mafunzo haya kwa mameneja miradi na wajumbe wakuu wa bodi za asasi za kiraia yamekuja baada ya kufanyika upembuzi yakinifu katika asasi hizi na kuonekana kwamba kuna umuhimu wa kuzipatia mafunzona kuzi Imarisha katika maeneo yote ya usimamizi wa miradi hasa eneo la utawala na uongozi bora kama ilivyo onekana katika matokeo ya upembuzi yakinifui “readiness review” yaliyofanywa ili kutambua uwezo wa asasi za kiraia katika nyanja mbalimbali.
Hatua hii ni utekelezaji wa lengo la nne la mradi wa EpiC “Kuzijengea uwezo asasi za kiraia na kuziwezesha kupata ufadhili wa moja kwa moja kutoka kwa wafadhili pamoja na utekelezaji wa miradi ya PEPFAR.”
“Wafadhili hawawezi kuweka hela nyingi kwenye mashirika yasiyo wajibika. Wajumbe wa bodi, wakurugenzi na meneja ni lazima kuwajibika kwenye mambo yote katika shirika.” Alisema Bernard Ogwang, Mkurugenzi wa Mradi wa EpiC.
Wakurugenzi na meneja wa mashirika, wasimamizi wa fedha na wajumbe wakuu wa bodi mbali na kuhudhuria mafunzo haya ya utawala na uongozi bora, pia wamekutana na wakuu wengine kutoka kwenye asasi za kiraia mbalimbali ambapo wameshirikishana uzoefu wa namna bora ya kuongoza na kutekelezaji miradi ili kuhakikisha malengo yanafikiwa.
“Niko kwenye bodi kwa zaidi ya miaka kumi ila hatujawahi kupata mafunzo ya utawala na uongozi bora. Mafunzo haya yameleta chachu na mwanga, yatabadili utekelezaji wetu ikiwemo uwajibikaji wa bodi na kufuatilia utekelezaji wa miradi.” alisema Juma Mwesigwa, Mkurugenzi wa asasi ya HUHESO.
EpiC ni mradi wa kimataifa wa miaka mitano unaotekelezwa na shirika la FHI360 kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) pamoja na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), uliojikita katika kufikia na kuendeleza udhibiti wa janga la VVU/UKIMWI katika Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hii ni kupitia kutoa msaada wa kitaalamu na huduma za moja kwa moja katika kuondoa vikwazo vilivyopo kufikia 95-95-95, na kuhamasisha usimamizi wa kujitegemea wa miradi ya VVU/UKIMWI kitaifa kwa kuboresha programu za utambuzi wa hali ya maambukizi ya VVU, kinga, matunzo na tiba.
No comments:
Post a Comment