WAKAZI wa Kata ya Minziro,Jimbo la Nkenge,wilaya ya Missenyi, mkoani Kagera wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Balozi Liberata Mulamula wamefanikisha kupatikana kwa kiasi cha Shilingi Milioni 12.7 katika Harambee ya kuchangia Bweni la wasichana.
Kiasi hicho cha fedha kimelekezwa kwa ajili ya shughuli za Maendeleo katika sekta ya Elimu,Katani hapo,hususani ujenzi huo wa bweni ili kuhakikisha wasichana wanasoma kwa utulivu na kufanya vyema katika masomo yao.
Harambee hiyo iliyofanyika mwishoni mwa siku za kufunga mwaka na
kuhudhuriwa na mgeni rasmi,Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki,Balozi Liberata Mulamula,kilipatikana kiasi hicho na
kukielekeza sekta ya elimu Sekondari.
Katika harambee hiyo,ambayo Balozi Mulamula,alichanga kiasi cha
Shilingi Milioni Mbili, zilipatikana Shilingi milioni Mbili, Laki Saba na elfu
sabini na tisa ( 2,779,000/-) zikiwa pesa taslimu,Shilingi Milioni Kumi na Elfu
Ishirini ( 10,020,000/-) ahadi, huku mchanga ukiwa tripu 15 na mawe tripu sita.
Akiongea neno la utangulizi kabla ya kufanyika harambee
hiyo,Mratibu wa shughuli hiyo,ijulikanayo kwa jina la “Minziro Day”,Novath
Rukwago,alisema chimbuko lake linatokana na wazaliwa wa Kata hiyo, wanaoishi na
kufanya shughuli mbalmbali katika maeneo kadhaa ya nchini na nje ya nchi.
Rukwago alisema shughuli hiyo itakuwa endelevu kila mwaka kwa
tarehe na mwezi, lengo likiwa ni kukutana na kushirikisha mawazo baina yao na
wakazi wa kata hiyo kwa kubainisha changamoto zinazokabili kata na kuzipatia
ufumbuzi utakaokuwa chachu ya kujipatia Maendeleo.
“ Na baada ya kushirikishana na ndugu zetu wanaoishi katika Kata
hii, tukaona tuanze na changamoto ya kutatua katika sekta ya elimu sekondari
kwa kuchangia ujenzi wa bweni la wasichana Sekondari ya Minziro,”alisema
Rukwago.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nkenge,Frolent Kyombo, aliwataka
mipango inayoibuliwa na wana Minziro wanaoishi nje, wakawashirikisha
wawakilishi wa wananchi ili kurahisisha kufikia maendeleo kwa haraka.
Aidha Waziri Mulamula, licha ya kuwapongeza aliwatia nguvu na
kuwaasa kuiboresha zaidi shughuli hiyo ili iweze kuleta tija katika kata hiyo, wilaya, mkoa wa Kagera na nchi kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment