Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe Dkt. Dorothy Gwajima ameitambulisha rasmi Wizara yake kwa Umma na kuwahakikishia kuwa itafanyika kuwa mwanga katika kuongeza kasi kwenye Maendeleo ya Jamii.
Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo tarehe 17 Januari, 2022 Jijini Dodoma kwenye Ofisi za Wizara zilizoko Mji wa Serikali, Mtumba wakati akizungumza na Menejimenti ya Wizara hiyo katika kikao cha kwanza kukutana tangu kuanzishwa kwa Wizara hiyo Mpya.
Amesema kuwa Wizara ipo tayari kutekeleza majukumu yake sambamba na maagizo mbalimbali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kufikia azma yake ya kuwaletea wananchi Maendeleo.
"Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameona umuhimu wa kuwepo kwa Wizara Ili iweze kuratibu na kuhakikisha wananchi wa makundi yote wanashiriki kusukuma maendeleo ya Taifa lao Sekta zote" alisema Dkt. Gwajima
Waziri Dkt. Gwajima ameongeza kuwa Wizara yake itashirikiana na wananchi na wadau wote katika kuhakikisha kuwa inakuwa kiungo katika kuhakikisha Jamii inakuwa na maendeleo na Ustawi.
Hatua hii inakuja mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuanzisha Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum yenye lengo la kuhakikisha jamii inapata Maendeleo na Ustawi wao.
No comments:
Post a Comment