WANAFUNZI 102 KIDATO CHA NNE WAFUTIWA MATOKEO - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday, 15 January 2022

WANAFUNZI 102 KIDATO CHA NNE WAFUTIWA MATOKEO

 BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya mitihani ya Kidato cha Nne,huku likiwafutia   watahiniwa 102 waliobainika kufanya udanganyifu katika mitihani hiyo iliofanyika mwishoni mwa 2021, huku ikibainika udanganyifu ukiongezeka tofauti na mwaka 2020.




Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu wa NECTA, Dkt. Charles Msonde,wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. 



Dkt. Msonde alisema udanganyifu umefanywa na baadhi ya watahiniwa  waliofanya mitihani katika madarasa ya mitihani ya Kitaifa,kwa kuibainisha udanganyifu kufanywa na watahiniwa 83   wa Upimaji wa kitaifa wa darasa la nne, 27 ni wa upimaji wa kitaifa wa kidato cha pili.

 

 

“102 ni wa mtihani wa kidato cha nne na watahiniwa wawili ni wa mtihani wa maarifa,” amesema Dkt. Msonde.



Alibainisha kuwa ikilinganishwa na matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2020, mwaka huu wanafunzi wengi zaidi walihusika kufanya udanganyifu kwenye mitihani ya kidato cha nne ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 27.



Mwaka jana, ni wanafunzi 75 tu ndiyo walifanya udanganyifu katika mtihani huo.



Baraza hilo limesema limefuta matokeo ya wanafunzi hao kwa mujibu wa kifungu cha 5 (2) (i) na (j) cha sheria ya Baraza la Mitihani sura ya 107 kikisomwa pamoja na Kifungu cha 30(2) (b) 2016 cha Kanuni za Mitihani.



NECTA pia imezuia matokeo ya wanafunzi 555 ambao walipata matatizo ya kiafya na hivyo kushindwa kufanya mitihani yote au baadhi.



“Watahiniwa wahusika wamepewa fursa nyingine ya kufanya upimaji wa mtihani hii ya kitaifa mwaka huu wa 2022,” amesema Dkt.Msonde.



Amesema, kati ya watahiniwa 483,820 wasichana waliofaulu 218,174 sawa na asilimia 85.77 huku wavulana wakiwa 204,214 sawa na asilimia 89.00 wamefaulu.



“Mwaka 2020 watahiniwa 373,958 sawa na asilimia 85.84 wa shule walifaulu mtihani huu. Hivyo ufaulu wa watahiniwa wa shule umeongezeka kwa asilimia 1.46 ikilinganishwa na mwaka 2020,” amesema.



Dkt. Msonde amesema, katika matokeo hayo Shule ya Kemebos ya Kagera imeshika nafasi ya kwanza katika 10 bora kitaifa ikifuatiwa na shule za St. Francis (Mbeya), Waja (Geita), Bright Future Girls (Dar es Salaam) Bethel Sabs Girls (Iringa), Mau Seminary (Kilimanjaro) na Feza Boys’ (Dar es Salaam).



Shule nyingine ni Precious Blood ya Mkoa wa Pwani, Feza Girls’ (Dar es Salaam) na Mzumbe ya mkoani Morogoro.

 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso