Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa OR TAMISEMI anayeshughulikia sekta ya elimu Gerald Mweri amesema Serikali imejipanga kuondoa adha kwa wanafunzi shule za msingi kutembea umbali mrefu kwa kujenga madarasa 3000 katika vituo shikizi 970 na kuzisajili kuwa shule kamili.
Ameyabainisha hayo Jijini Dodoma wakati akifunga mkutano wa mwaka wa wadau wa elimu waliokutana kutathmini hali ya sekta ya elimu na kuweka mikakati mipya ya namna ya kuboresha elimu amesema kwa sasa serikali kupitia fedha za IMF za kujenga madarasa 15000 madarasa 3000 yatajengwa kwenye shule shikizi katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
“Tunaamini tukishajenga madarasa 3000 kwenye hizi vituo shikizi 970 tunaamini tunakwenda kuweka historia tena kubwa kwa shule hizi za msingi mpya 970 pia tutakuwa tumewaondolea adha kubwa watoto kutembea umbali mrefu” amesema Mweri.
Amesema Serikali imeondoa vikwazo vingi vilivyokuwa vikiikabili sekta ya elimu hasa katika uhaba wa walimu wa masomo ya Sayansi na serikali iliajiri walimu wa masomo ya Sayansi takribani 3000 wote hawa tuliwapeleka maeneo yenye uhaba mkubwa wa walimu hao.
“Mwanzo tulikuwa tunaajiri walimu na kuwapeleka kwenye Halmashauri lakini utaratibu wa sasa walimu waliomba sehemu zenye uhaba tu na mwalimu alikuwa anajipangia shule mwenyewe kwa kuwa shule hizo tuliziweka kwenye mfumo na mwaka huu hatukua na malalamiko upangwaji wa sehemu za kufundisha” amesema Mweri.
Pia amebainisha kuwa katika sehemu ya udhibiti ubora wa elimu nako serikali imefanya makubwa kwa sasa idara hiyo inafanya kazi nzuri na inatambulika na wazazi na wadau wa elimu wanajua kazi ya idara hiyo huku akiwataka wadau na wazazi kuitumia idara hiyo ipasavyo ikiwamo kujua kazi zinazofanyika katika shule hizo.
Akizungumzia mkutano huo amesema maoni mengi ya wadau tayari serikali ilishaanza kuyafanyia kazi na kwamba maoni hayo watayafanyia kazi na kuyajumuisha katika kuboresha sera za elimu na kuwataka wadau hao kuendelea kutoa maoni yao ya namna ya kuboresha sekta ya elimu.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe amesema kupitia mkutano huo wamefanya tathmini ya utendaji katika sekta ya elimu kwa kushirikiana na wadau na wamepokea maoni mbalimbali ya wadau na watayafanyia kazi ipasavyo katika kuboresha sekta ya elimu.
“Tunaamini mkutano huu utaleta majibu mazuri kutokana na michango ya wadau mbalimbali ikiwa ni serikali, wadau wa maendeleo, mashirika na wale ambao wako moja kwa moja wanaofundisha katika shule na vyuo” amesema Prof. Mdoe.
Nao baadhi ya wadau wa elimu akiwamo mkurugenzi wa shirika la Hakielimu Dkt. John Kalage amesema anaamini kupitia mkutano huu wa siku mbili na mijadala na maada zilizowasilishwa sekta ya elimu itakwenda kuboreshwa kwa kiasi kikubwa sana na mpaka sasa sekta hiyo imepiga hatua kubwa sana.
“Kupitia mkutano huo umeonyesha ni kiasi gani Serikali kupitia Wizara ya elimu imejipanga kikamilifu katika kuboresha hali ya elimu hapa nchi ili iwe na muendelezo mzuri na kuzalisha wanafunzi wenye ujuzi” amesema Dkt. Kalage.
Nae Mkurugenzi wa shirika lisilokuwa la kiserikali la Karibu Tanzania Organizationi Majdi Mzengwa amesema kunamafanikio makubwa sana katika sekta ya elimu hasa katika shule za kata zilizoanzishwa hapa nchini zimeleta mapinduzi makubwa kwani shule hizo ndizo kwa sasa zinalisha vyuo vikuu kwa wanafunzi wengi wanaotoka shule za kata wanafika vyuo vikuu licha kuwa mwanzo zilibezwa sana.
Kwa upande wake Mdhibiti ubora wa shule kanda ya magharibi Bi. Edith Mwijage amesema kumekuwa na maboresho makubwa katika ofisi ya udhibiti ubora wa shule kwani mwanzo hawakuwa na ofisi lakini kwa sasa wanaofisi nzuri na vitendea kazi ikiwa ni pamoja na usafiri wa kufika katika maeneo ya shule
No comments:
Post a Comment