OFISI ZA ARDH MIKOA ZAONGEZA BAJETI YA WIZARA ASILIMIA 44 - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday, 22 November 2021

OFISI ZA ARDH MIKOA ZAONGEZA BAJETI YA WIZARA ASILIMIA 44




Na Mwandishi Wetu, DODOMA
Tangu kuanzishwa kwa Ofisi za Ardhi za Mikoa, bajeti ya wizara ya Wizara Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeongezeka kutoka shilingi Bilioni 67 kwa mwaka wa fedha 2020/2021 mpaka kufikia Bilioni 97 mwaka 2021/2022.

Hilo ni ongezeko la asilimia 44 na kuyafanya majukumu ya wahasibu wa kuongezeka maradufu katika kutekeleza kazi za wizara kwenye Ofisi za Mikoa na halmashauri zake.

Hayo yamebainishwa tarehe 20 Novemba 2021 jijini Dodoma na Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Walter Lungu wakati akifungua kikao kazi cha kujadili changamoto na namna ya kuongeza ufanisi katika utendaji kazi kwa wahasibu ili wawe sehemu ya kuchangia kufanikisha lengo la mapato ambapo wizara ya Ardhi imepangiwa kukusanya shilingi Bilioni 221 kutoka bilioni 180 za mwaka wa fedha uliopita 2021/2021.

Pamoja na masuala mengine ya kiutendaji, Bw. Lungu alizungumzia suala la wahasibu kujiendeleza kwa lengo la kuhakikisha huduma katika sekta ya ardhi inatolewa kwa wepesi, haraka na kwa ufanisi wa hali ya juu.

"Kutokana na maendeleo kwenye teknolojia kuathiri kada mbalimbali katika utuomishi wa umma ikiwemo kada ya wahasibu mnatakiwa kujiendeleza ili kuhakikisha huduma inatolewa kwa wepesi, haraka na kwa ufanisi wa hali ya juu". Alisema Lungu

Akimuwakilisha Kamishna wa Ardhi nchini katika kikao hicho, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Usimamizi na Uratibu Bw. Wilson Luge aliwataka wahasibu kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi bila ya kuhofia cheo au nani alitoa maelekezo kwani hoja ya uhasibu itakapokuja kuhusu matumizi yasiyo rasmi ya fedha haitaangalia nani alitoa maelekezo bali ni utaratibu gani ulitumika katika kutekeleza majukumu na kama sheria na taratibu zilifuatwa kwenye taaluma ya uhasibu.

Pia Luge aliwaomba Wahasibu washirikiane kwa ukaribu na Makamishna wa Mikoa wakati wa kuandaa bajeti ili kuepuka makossa yanayojitokeza mara kwa mara aliyoyaeleza kuwa, wakati mwingine yanakwamisha utengaji fedha kwa majukumu yaliyokusudiwa.

Akitoa salamu kwa niaba ya Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Ardhi, Bw. Antony Mgeni ambaye ni Afisa Rasilimali Watu Mwandamizi alisisitiza umuhimu wa Wahasibu kuheshimu misingi ya taaluma sambamba na kujikita katika maadili kwa lengo la kuepusha makosa ya kitaaluma yanayoweza kujitokeza.

Mgeni aliongeza kuwa, kumekuwa na migongano ya hapa na pale miongoni mwa wahasibu katika Wizara hivyo aliwataka kutumia nafasi ya kikao hicho kujadili tofauti zao binafsi na kupendana ili wawe na furaha mahali pa kazi kwani maelewano mabaya yanasababisha kushindwa kukamilika kwa kazi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso