Ripoti mpya imeonyesha kwamba Ulaya bado inajikongoja katika masuala ya usawa wa kijinsia katika miaka ya hivi karibuni na kuonya kwamba hali inaweza kusalia hivyo kutokana na janga la COVID-19.
Ripoti hii mpya imechapishwa jana Alhamisi. Kulingana na ripoti hiyo, pengo kubwa zaidi la usawa bado linasalia kwenye nafasi za uongozi, kwa kuwa wanawake bado ni wachache kwenye nafasi za kimamlaka.
Umoja wa Ulaya kwa ujumla ulipata pointi 68 kati ya 100 katika ripoti hiyo ya Usawa wa Kijinsia iliyohapishwa na Taasisi ya Ulaya ya Masuala ya Usawa wa Jinsia, EIGE.
Kiwango hicho hata hivyo kinaashiria ongezeko la pointi 0.6 tu ikilinganishwa na mwaka 2020, na pointi 5 katika kipindi cha miaka 11.
Sehemu ya ripoti hiyo imesema huku masuala ya usawa wa kijinsia yakisuasua, kwa kuongezeka pointi moja tu katika kipindi cha miaka miwili, itauchukua ulimwengu karibu vizazi vitatu kufikia malengo ya usawa wa jinsia, kwa kuangazia kasi ya sasa.
Imesema, janga la COVID-19, huenda likwa si tu kwamba limezorotesha mchakato wa kusonga mbele, bali pia linauweka kwenye hatari kubwa mpango mzima wa kufikia usawa wa jinsia.
Mkurugenzi wa EIGE Carlien Scheele amekiri kwamba Ulaya imepiga hatua ndogo katika masuala ya usawa wa jinsia, lakini mataifa yaliyo na kiwango cha chini zaidi kwa kiasi kikubwa kasi yaoiliathiriwa zaidi na janga la COVID-19. Changamoto za kiuchumi pia zinawaathiri kwa muda mrefu zaidi wanawake, huku muda wa kuishi kwa wanaume nao ukipungua.
Bado ni vigumu kwa wanawake kushika nafasi za uongozi kama wanawake hawa kansela Angela Merkel wa Ujerumani na rais wa halmashauri ya Ulaya, Ursula von der Leyen.
Amesema, idadi kubwa ya wanawake ni watoa huduma za afya na hivyo wengi hujikuta katika hatari ya kuambukizwa virusi vya corona, na wakati huohuo, wanaume wakiwa hatarini zaidi kuugua na kulazwa hospitalini kutokana na maambukizi ya COVID-19.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa hata kwenye maeneo kazi, na hata afya pia kumeathirika na hatua zinazopigwa ni ndogo mno. Mzigo mkubwa mara nyingi unabebwa na mwanamke kuanzia kazi za nyumbani ambazo hazina malipo hadi malezi ya watoto na hasa wakati mataifa yalipokuwa yakitekeleza vizuizi vya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona kama vya kufunga shughuli.
Mataifa matatu yanayoongoza kwa usawa wa kijinsia miongoni mwa wanachama wa Umoja wa Ulaya ni Sweden, Denmark na Uholanzi. Ugiriki ilikuwa ya mwisho kwa alama 52.5, ikifuatana na Hungary na Romania.
Ujerumani ilijiimarisha kidogo na kuvuka kiwango cha Umoja wa Ulaya kwa alama 68.6, ikiwa ni pamoja na pointi 6 za tangu mwaka 2010.
Luxembourg lilikuwa ni taifa lilijiimarisha kwa kiasi kikubwa zaidi katika masuala ya usawa wajinsia, na Slovenia ilikuwa taifa pekee mwanachama wa umoja huo kurudi nyuma tangu mwaka 2018.
Italia na Malta pia zimeonekana kujiimarisha zaidi katika muongo uliopita, wakati kukishuhudiwa hatua finyu nchini Poland, Hungary na Jamhuri ya Czech.
No comments:
Post a Comment