Watendaji katika sekta ya Ardhi nchini wametakiwa kuwajibika kwa kufanya kazi kwa bidii kwa kuhakikisha wanatoa hati kwa wamiliki wa ardhi sambamba na kuhamasisha ukusanyaji kodi ya pango la ardhi.
Agizo hilo lilitolewa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Angeline Mabula,wakati akizungumza na watumishi wa sekta ya ardhi mwishoni mwa wiki kwenye ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mara.
Dkt Mabula alisema ufanyaji kazi kwa kujituma kwa watumishi wa sekta hiyo itaiwezesha wizara ya ardhi kuongeza kasi ya utoaji hati na wakati huo kukusanya mapato yatokanayo na kodi ya ardhi.
Naibu Waziri wa Ardhi,alitanabaisha kwamba kwa sasa katika mkoa huo Mara kasi ya utoaji hati za ardhi pamoja na makusanyo yatokanayo na kodi ya ardhi hairidhishi na juhudi kubwa zinahitajika katika kutoa hati na kuhamasisha wamiliki kulipa kodi ili serikali iweze kupata fedha za kuendesha shughuli zake mbalimbali.
Kwa mujibu wa
Taarifa ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mara Bi. Hapiness Mtutwa katika
kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 uliweza kukusanya shilingi bilioni 1.065
sawa na asilimia 23 katika malengo ya bilioni 4 huku mwaka wa fedha 2020/2021
ukikusanya bilioni 1.7 sawa na asilimia 47.5 kati ya malengo bilioni 3.7.
‘’Maelekezo yangu mkafanye kazi kwa bidii katika wilaya zenu na nikikuta
mtendaji wa sekta ya ardhi hafanyi haya ninayoelekeza basi ujue wewe
hutufai’ alisema Dkt Mabula
Mkurugenzi Msaidizi idara ya Maendeleo ya makazi Wizara ya Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Bi. Imaculata Senje aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi
hasa wale wa Mipango Miji kuwa wabunifu kwa kuwaelimisha wananchi umuhimu wa
maeneo yao kupimwa.
‘’Kuna miji midogo inakuwa kwa kasi katika maeneo yenu na inawezekana kama
Afisa Mipango Miji ukasema huna kazi lakini unaweza kuanza kwa ktuoa elimu kwa
mtu mmoja mmoja ukieleza umuhimu wa eneo lake kupangwa na kupima na
kumilikishwa’’ alisema Bi. Senje.
Naye Afisa Kodi Kutoka Wizara ya Ardhi Rehema Kilonzo aliwaeleza watendaji wa
sekta ya ardhi katika mkoa wa Mara kuhakikisha wanayajua na kufuatilia kwa
karibu madeni ya wadaiwa wote sugu wa kodi ya pango la ardhi na kubainisha
kuwa, pamoja na Wizara kuelewa changamoto zilizopo kwenye mfumo lakini bado
watendaji hao wana nafasi ya kujua madeni halisi ya wadaiwa na hivyo kuwafanya
kuwa katika sehemu salama kwenye utendaji wao.
No comments:
Post a Comment